1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Ureno leo

18 Juni 2008

Katika robo-finali ya kombe la Ulaya Ujerumani ina miadi leo na wareno.

https://p.dw.com/p/EMJO
Lukas Podolski atacheza leo ?Picha: picture-alliance / Sven Simon

Ujerumani,mabingwa mara 3 wa dunia na Ulaya,wanarudi uwanjani jioni ya leo kupambana na Ureno ikiwa haina uhakika ya kucheza na mastadi wake 2-Torsten Frings na Lukas Podolski.

Mpambano huu wa kukata na shoka, utachezeshwa na rifu Frojdfeldt kutoka Sweden.

Kesho ijumaa, itakua zamu ya Croatia na Uturuki kuteremka uwanjani kabla jumamosi Holland haikukata tiketi yake ya nusu-finali.

Mabingwa wa dunia Itali, wana miadi na jirani zao Spian jumapili hii wakikamilisha duru hii mpya inayoanza leo ya robo-finali.

Nani atamzuia chipukizi wa Ureno Christiano Ronaldo asiufumanie leo mlango wa Ujerumani, ndilo swali linalomuumiza kichwa kocha wa Ujerumani Joachim Loew. Ronaldo mwenye umri wa miaka 23 anaangaliwa sasa ndie mchezaji bora kabisa wa dimba ulimwenguni-nyota ya Ronaldinho wa Brazil ikiwa imefifia.

Kocha wa Ureno,mbrazil Filipe Scolari, anaiheshimu sana Ujerumani.Alisema kabla changamoto ya leo kwamba anapenda kuangalia jinsi Ujerumani inavyocheza dimba na anavutiwa na mbinu zake za mchezo.Scolari, anadai kwamba hahadaiki na kuanza vibaya Ujerumani,kwani ni tabia yake ,lakini kila mashindano yakiendelea, Ujerumani hufufuka na kupata nguvu.Hata Christiano Ronaldo amesema anaiheshimu Ujerumani ,kwani asema ni timu kali na iliopevuka.

Franz Beckenbauer, aliekua nahodha wa timu ya Ujerumani na kocha wake ilipotawazwa mabingwa wa dunia 1974 na 1990,anadai Ujerumani, haiwezi kutamba leo mbele ya Ureno.

Kumekuwapo na shaka-shaka iwapo wachezaji 2 maarufu katika kikosi cha nahodha Michael Ballack -Torston Frings alievunjika mbavu na Lukas Podolski alieumia wataweza kucheza .

Kocha Joachim Loew, anasubiri hadi dakika za mwisho kuamua hatima yao.Ni Lukas Podolski anaetakiwa na klabu 2 za nje-Juventus ya itali na Tottenham ya Uingereza, alietia mabao 3 ya Ujerumani hadi sasa katika kombe hili la Ulaya.

Kutocheza Podolski leo,kutaiumiza sana Ujerumani.

Pale Ujerumani ilipocheza na Ureno mara mwisho, Christiano Ronaldo hakuwika mbele ya wingi mwengine hatari wa Ujerumani, Bastian Schweinsteiger ambae kama Ronaldo ana umri wa miaka 23 na ameshakomea mabao 13 kwa timu ya taifa.