1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuisaidia Moldova kukabiliana na wakimbizi

5 Aprili 2022

Ujerumani imetangaza mjini Berlin kuwa itatoa mkopo wa yuro milioni 50 kwa Moldova sambamba na msaada wa milioni 40 ili kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na wimbi la wakimbizi kutoka Ukraine.

https://p.dw.com/p/49V6N
Deutschland | Moldau-Konferenz in Berlin
Picha: Florian Gaertner/photothek/picture alliance

Msemaji wa serikali Steffen Hebestreit amesema Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ametangaza mkopo huo wakati wa mkutano wa kimataifa wa wafadhili kwa ajili ya Ukraine. Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano wa Ufaransa na Romania.

Mkopo huo unalenga sio tu kuwasaidia wakimbizi wa Ukraine lakini pia kutoa msaada mpana wa kifedha na kukabiliana ongezeko la gharama za nishati. Hebestreit amesema, hakuna nchi hadi sasa ambayo kulingana na idadi ya raia wake, imewapokea wakimbizi zaidi kutoka Ukraine kuliko Jamhuri ya Moldova.Wakimbizi wa Ukraine wapindukia milioni 11

Moldova inaathirika sana kutokana na mzozo huu wa Urusi na Ukraine kwa sababu ilikuwa tegemezi kwa karibu asilimia 100 kwa gesi ya Urusi na bei ya gesi imepanda karibu mara nane katika kipindi cha miezi sita iliyopita huku mfumuko wa bei ukipanda hadi asilimia 18.

Kauli ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani

Republik Moldau Parlamentswahl 2021 | Chisinau | Maia Sandu, Präsidentin
Rais wa Moldova Maia SanduPicha: Vladislav Culiomza/REUTERS

Katika mkutano huo, Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema wanataka kuimarisha ushirikiano na Moldova kwa muda mrefu: " Watu wote wana haki ya kuamua mustakabali wao wenyewe. Hakuna mtu anayepaswa kuishi kwa huruma ya jirani yake mwenye nguvu, iwe watu wa Ukraine au wa Moldova. Ndiyo maana tunataka kuimarisha ushirikiano wetu na Moldova kwa mahitaji ya haraka na kwa muda mrefu. Pamoja na washirika wetu wa Moldova tunataka kutathmini jinsi tunavyoweza kusaidia kupunguza utegemezi wa Moldova kwa Urusi kiuchumi, kifedha na kwa kuzingatia mahitaji ya nishati, kuimarisha ustahimilivu wa nchi hiyo."Ukraine, Georgia na Moldova zatiliana saini na Umoja wa Ulaya

Msaada huo ni pamoja na fedha kwa ajili ya maendeleo ya kijamii, miundombinu, shule na nyumba za makazi kwa manispaa zinazowapokea wakimbizi na lengo jengine kuwasaidia wanafunzi kutoka Ukraine kujumuishwa katika mfumo wa mafunzo ya taaluma ya nchi hiyo.

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, atasafiri kuelekea Kyiv wiki hii kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy. Msemaji wake, Eric Mamer, amesema leo Jumanne kwamba safari hiyo itafanyika kabla ya mkutano maalum wa kukusanya misaada huko Warsaw mwishoni mwa juma. Ni safari ya pili ya maafisa wa ngazi za juu wa EU nchini Ukraine. Wiki iliyopita Rais wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola alikuwa nchini humo.

Kulingana na data za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, idadi ya watu waliyoikimbia Ukraine na kwenda nchi zengine tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi wanakadiriwa kufikia milioni 4.2.