Ukraine, Georgia na Moldova zatiliana saini na Umoja wa Ulaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ukraine, Georgia na Moldova zatiliana saini na Umoja wa Ulaya

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya na wa nchi za Ulaya Mashariki leo wametiliana saini mikataba ya kibiashara na kiuchumi, huku Urusi ikitishia kuchukua hatua ili kuulinda uchumi wake.

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine akisaini mkataba wa ushirikiano na Umoja wa Ulaya mjini Brussels tarehe 27 Juni 2014.

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine akisaini mkataba wa ushirikiano na Umoja wa Ulaya mjini Brussels tarehe 27 Juni 2014.

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine amesema mkataba wa biashara na uchumi alioutia saini na Umoja wa Ulaya ni hatua muhimu kabisa kuwahi kuchukuliwa na Ukraine tokea nchi hiyo ijiondowe kwenye Shirikisho la Umoja wa Kisovieti.

Kwa mujibu wa mkataba huyo, biashara baina ya nchi hizo tatu na Umoja wa Ulaya itakuwa huru na itafanyika bila ya ushuru au vizingiti vya aina yoyote. Nchi hizo tatu za Ulaya mashariki zina bidhaa na huduma zinazotimiza viwango vya Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya pia utanufaika kwa kuuza bidhaa na huduma katika nchi hizo kwa urahisi. Rais wa Ukraine amesema ukurasa mpya wa historia umefunguliwa kwa nchi yake.

Urusi yatoa vitisho

Rais Vladimir Putin wa Urusi ambaye nchi yake imeonya juu ya makubaliano haya kati ya Umoja wa Ulaya na mataifa matatu yaliyowahi kuwa sehemu ya Shirikisho la Kisovieti.

Rais Vladimir Putin wa Urusi ambaye nchi yake imeonya juu ya makubaliano haya kati ya Umoja wa Ulaya na mataifa matatu yaliyowahi kuwa sehemu ya Shirikisho la Kisovieti.

Lakini Urusi imesema kuwa mikataba iliyotiwa saini baina ya Umoja wa Ulaya na nchi hizo tatu za Ulaya Mashariki itakuwa na madhara makubwa. Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov, ameeleza kuwa nchi yake itachukua hatua za kuulinda uchumi wake ikiwa itaathirika na mikataba hiyo. Ukraine, Georgia na Moldova sasa zimesogea karibu zaidi na Umoja wa Ulaya.

Aliyekuwa rais wa Ukraine, Viktor Yanukovych, hapo awali alikataa kuutia saini mkataba wa ushirikiano na Umoja wa Ulaya Novemba 2013, uamuzi ambao hatimaye ulimsababisha upinzani mkubwa kumfanya akimbilie Urusi.

Ni katika muktadha wa matukio hayo kwamba Urusi iliamua kulichukua jimbo la Krimea la Ukraine na kuliingiza katika himaya yake.

Wajumbe wa OSCE waachiwa

Waasi wanaotaka kujitenga kwa jimbo la Donezk, mashariki mwa Ukraine.

Waasi wanaotaka kujitenga kwa jimbo la Donezk, mashariki mwa Ukraine.

Katika kadhia nyingine kuhusiana na mgogoro wa Ukraine, Rais wa Uswisi, Didier Burkhalter, ambae pia ni Mwenyekiti wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya (OSCE) amepongeza hatua ya kuachiwa wajumbe wanne wa shirika hilo waliokuwa wametekwa nyara mashariki mwa Ukraine mwezi uliopita.

Hata hivyo, Burkhalter amesema wajumbe wengine ambao bado wanashikiliwa lazima pia waachiwe. Aliitoa kauli hiyo baada ya kiongozi wa watu wa mashariki mwa Ukraine wanaotaka kujitenga, kutangaza kwamba wajumbe hao wanne waliotekwa nyara mwishoni mwa mwezi Mei wameaachiwa na waasi.

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia Wakimbizi (UNHCR) limearifu kwamba idadi ya watu wanaokimbia mashariki mwa Ukraine imeongezeka. Hadi wiki iliyopita watu zaidi ya 16,000 walizikimbia sehemu za mashariki. Shirika hilo pia limesema kwamba kwa sasa wapo wakimbizi wa ndani 54,000 nchini Ukraine.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com