Uingereza, Australia na Canada zalitambua taifa la Palestina
21 Septemba 2025
Uingereza, Australia na Canada zimetangaza hii leo kulitambua rasmi taifa la Palestina katika mabadiliko makubwa ya miongo kadhaa ya sera za kigeni za nchi za magharibi na kuchochea hasira kutoka Israel. Ureno inatazamiwa kutangaza pia kulitambua taifa la Palestina baadae siku ya Jumapili, wakati Israel ikikabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa juu ya vita vyake vya Gaza, vilivyochochewa na shambulizi la Hamas Oktoba 7 2023. Katika tangazo lake kupitia ukurasa wa X, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema ili kufufua matumaini ya amani kwa Wapalestina na Waisraeli, na suluhisho la mataifa mawili, Uingereza inatangaza kulitambua rasmi taifa la Palestina. Uingereza na Canada zimekuwa nchi za kwanza za kundi la G7 kuchukua hatua hiyo, huku Ufaransa na mataifa mengine yakitarajiwa kufuata katika Mkutano Mkuu wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa unaofunguliwa Jumatatu mjini New York.