1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani leo Oktoba 19

Josephat Charo19 Oktoba 2005

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wamejihusisha na mkutano wa bunge jipya la Ujerumani na kuchaguliwa kwa rais mpya. Mada nyengine zinahusu vita dhidi ya homa ya ndege na kufunguliwa kwa maonyesho ya vitabu mjini Frankfurt.

https://p.dw.com/p/CHMV

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatufungulia kurasa za magazeti ya Ujerumani na kikao cha bunge jipya la Ujerumani. Gazeti linasema kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa kipindi cha uchaguzi bunge hilo sasa limeanza shughuli zake kwa utulivu – siku yake ya kwanza kukutana.

Lakini ikiwa bunge halitafikiria kuhusu jukumu lake, na kuanza kujidhihirisha kama makundi mbalimbali ya vyama vya kisiasa badala ya muungano, basi halitaweza kutoa ishara zinazotarajiwa na wananchi na kukubalika wala kutambuliwa, kama vile serikali iliyo na wingi wa wabunge inavyoheshimiwa.

Gazeti la Offenbach Post linakosoa kuongezeka kwa idadi ya makamu wa rais wa bunge kufikia sita. Mhariri anasema kwa kuwa Wolfgang Thierse hayuko tayari kung´atuka na chama cha SPD pamoja na muungano wa CDU-CSU vilikubaliana kuunda kiti chenginge cha makamu, basi sasa kwa mara ya kwanza rais wa bunge la Ujerumani ana wajumbe wengi. Vyama vya FPD, Kijani na chama cha mrengo wa kushoto, havingeweza kulizuia jambo hilo, kwa kuwa vyama vya SPD pamoja na muungano wa CDU-CSU viliibadili ajenda hiyo kwa mda mfupi kwa maslahi yao.

Gazeti la Märkische Oderzeitung limezungumzia kushindwa kwa mara ya tatu kwa mwenyekiti wa chama cha mrengo wa kushoto, Lothar Bisky, kuchaguliwa kwa wadhifa wa makamu wa rais wa bunge la Ujerumani. Gazeti linasema pengine halikuwa jambo la maana kumporomosha bwana Bisky mwenye umri wa miaka 64.

Zaidi ya hayo kiongozi huyo wa zamani wa chama cha SPD na kiongozi wa sasa wa chama cha mrengo wa kushoto, Oskar Lafontaine, wanatakiwa kujulishwa mapema upepo unakoelekea. Mchezo usioleweka utaendelea bungeni katika kipindi kijacho na chanzo cha malumbano ya chama cha mrengo wa kushoto lazima kitafutwe na mapema.

Gazeti la Rhein Neckar kutoka mjini Heidelberg lina maoni tofauti: Kushindwa kwa mara ya tatu kwa Lothar Bisky, ni kitendo ambacho bunge halina wajibu wowote wa kutoa msamaha. Ni jawabu kwa wanasiasa wa mrengo wa kushoto ambao wamejaribu kuingiza kwa hila mawazo ya kisoshalisti ya jamhuri ya kidemokrasia ya zamani, DDR, katika bunge.

Likitugeuzia mada, gazeti la Landeszeitung kutoka mjini Lüneburg limezungumzia hatua dhidi ya kuzuka kwa homa ya mafua hapa Ujerumani. Gazeti linasema wanasiasa wanaohusika na maswala ya afya hawana haraka ya kulishughulikia tatizo hili. Kwa sasa majimbo yote ya Ujerumani yana uwezo asilimia 50 wa kupambana na homa hiyo hatari.

Wakati huo huo, waziri wa afya, Ulla Schmidt, amezungumzia kuhusu matumaini kidogo ya chanjo dhidi ya homa hiyo. Uwezo wa chanjo hiyo kupambana na homa ya ndege ni duni kwa sababu, virusi wanaosababisha homa hiyo hubadilika mara kwa mara na kuwa na umbo lengine ambalo haliwezi kuangamizwa na dawa ya awali.

Gazeti la Tagesspiel limeonya dhidi ya wasiwasi mkubwa miongozi mwa raia. Linasema homa hiyo ni ugonjwa unaowaathiri ndege na wala sio binadamu. Pia hata kama virusi wanaosababisha homa hiyo wataingia katika mataifa ya magharibi, ni kuku, mabatamzinga na ndege watakaokuwa hatarini, na wala sio binadamu.

Kwa hofu ya kuambukizwa homa hii wajerumani wengi wanakimbilia kudungwa chanjo, jambo ambalo gazeti la Tagesspiegel limeliezea kuwa upuzi mtupu, likisema homa ya kawaida husababisha vifo vya wajerumani elfu 10 kila mwaka. Ikiwa chanjo dhidi ya homa itatumiwa, wasiwasi wa kuambikizwa homa ya ndege itawaathiri watu wengi zaidi kuliko idadi ya watu watakaoathiriwa na homa hiyo duniani kote.

Likitukamilishia udondozi wa magazeti ya leo, gazeti la Stuttgarter limezungumzia maonyesho ya vitabu yanayoendelea mjini Frankfurt hapa Ujerumani. Gazeti linasema kwa wakati huu maandishi yaliyochapishwa ni mojawapo ya njia za kuuhamasisha umma kuhusu habari na matukio mbalimbali.

Mda mrefu kabla ya toleo la sita la kitabu cha Harry Porter kuuzwa katika maduka ya Ujerumani, kulikuwepo na ukalimani katika lugha mbalimbali kwenye mtandao wa mawasiliano wa internet. Na mda mfupi baada ya vitabu kutolewa, filamu ya kwanza ikaonyeshwa na vitabu vya kwanza vya kusikiliza mfano wa redio vikauzwa.

Mashindano haya hata hivyo, hayatakiwi kuiharibu biashara ya makapuni ya kuchapisha vitabu, kwani watu wanaosoma vitabu vingi hupendelea pia kutumia njia nyengine za mawasiliano.