1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchina yatetea uwekezaji wake barani Afrika

13 Mei 2010

China imetetea sera zake za uwekezaji barani Afrika,kufuatia ripoti zinazosema kuwa nchi hiyo imetia saini mkataba wa mamilioni kujenga kiwanda cha saruji nchini Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/NMjw
South African President Thabo Mbeki, right, and his Chinese counterpart, Hu Jintao, left, stand during a welcoming ceremony in Pretoria, South Africa, Tuesday, Feb. 6, 2007. Hu is on a state visit to South Africa as part of his African tour. (AP Photo/Denis Farrell)
Rais wa China Hu Jintao(kushoto) na rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki.Picha: AP

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Financial Times, China hiyo kesho itatangaza mpango mkubwa kabisa wa uwekezaji kwa miaka miwili ijayo nchini Afrika Kusini. Mradi huo unahusika na ujenzi wa kiwanda cha saruji na utagharimu kama dola milioni 220.Kuambatana na makubaliano hayo,shirika linalodhibitiwa na serikali - China Africa Development Fund na kampuni ya Kichina- Jidong Development Group - zitasaidia kujenga kiwanda hicho cha saruji nje ya jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Katika miaka ya hivi karibuni, China imekuwa ikiimarisha uhusiano wake wa kibiashara na kiuchumi na nchi za barani Afrika na hali hiyo, imezusha lawama kutoka nchi za Magharibi kuwa China sasa ina mtazamo wa kile kilichoitwa"ukoloni mambo leo" kuelekea bara la Afrika. China vile vile imekosolewa kuwa katika uhusiano wake na serikali za Sudan na Zimbabwe, inatanguliza zaidi maslahi yake ya kujipatia malighafi inayohitajiwa kuendeleza ukuaji wa kiuchumi nchini mwake. Duniani, uchumi wa China unachukua nafasi ya tatu.

"Uwekezaji wa China barani Afrika,unazidi kuzingatia mahitaji ya masoko. Makampuni mengi na ya kila aina yanawekeza barani Afrika katika sekta mbali." Hiyo ni kwa mujibu wa Makamu wa Waziri wa Biashara wa China, Fu Ziying.Katika mahojiano yake na jarida la kiuchumi Wall Street Journal Fu amesema,biashara inayofanywa na China barani Afrika, mwaka huu itapindukia dola bilioni mia mojo. Na katika miaka mitano ijayo, kiwango cha uwekezaji huenda kikaweka rekodi mpya.

Kuambatana na makubaliano ya mwaka 2007, Benki ya viwanda na biashara ya China imewekeza dola bilioni 5.5 katika benki ya Afrika Kusini, "Standard Bank". Hadi sasa, hicho ni kiwango kikubwa kabisa cha fedha kupata kuwekezwa na China barani Afrika. Uwekezaji huo, umechukua takriban robo ya fedha zilizotengwa na China kwa ajili ya bara la Afrika.

Kwa upande mwingine, tarakimu rasmi za China zinaonyesha kuwa, thamani ya biashara yake barani Afrika mwaka jana ilifikia dola bilioni 91. Kulinganishwa na mwaka uliotangulia huo ni upungufu wa asilimia 17.6 uliosasbabishwa na mgogoro wa kiuchumi duniani.

Mwandishi:P.Martin/AFPE

Imepitiwa na: Hamidou,Oummilkheir