Uchaguzi jimboni North-RheinWestphalia | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 09.05.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Uchaguzi jimboni North-RheinWestphalia

Wajerumani wanapiga kura hii leo katika jimbo la North-Rhein Westphalia lililo na wakazi wengi zaidi hapa nchini.Kiasi cha wapiga kura milioni13.5 wamesajiliwa na wanatarajiwa kushiriki katika shughuli hiyo ya leo.

default

Bango la wagombea nyadhifa katika jimbo la North-Rhein Westphalia

Uchaguzi huu ni unafanyika ikiwa ni miezi michache tangu Kansela Angela Merkel aanze muhula wake wa pili serikalini.

Chama cha  Kansela Merkel cha CDU pamoja na  chama shirika  cha FDP kinachounga mkono masuala ya biashara sharti vipate ushindi katika  uchaguzi wa leo ndipo viweze kuwa na  wingi wa  kura  katika baraza la  wawakilishi wa majimbo, Bundesrat.Uchaguzi  huu unatazamwa kama kura ya maoni inayoitathmini serikali ya Angela Merkel iliyoingia madarakani yapata miezi sita iliyopita.Kwa mujibu wa mdadisi wa masuala ya  siasa katika chuo kikuu cha  hapa mjini Bonn,Gerd Langguth,uchaguzi huu una umuhimu mkubwa kwani unamtathmini  Kansela Merkel  mwenyewe.

TV Duell Jürgen Rüttgers gegen Hannelore Kraft Flash-Galerie

Waziri Mkuu wa jimbo la NRW Jürgen Rüttgers (CDU) katika mdahalo na Hannelore Kraft (SPD) kabla ya uchaguzi

Muungano wa  mrengo wa shoto na  kati


Uchumi wa jimbo la North-Rhein Westphalia ni mkubwa na ni sawa na  ule  wa mataifa ya Poland na Jamhuri  ya Czech kwa pamoja.Endapo vyama shirika vya CDU na FDP vilivyo madarakani havitashinda katika uchaguzi wa leo,ukosefu wa uwakilishi mkubwa katika baraza la wawakilishi  wa majimbo  Ujerumani, Bundesrat huenda ukasababisha utekelezaji wa sera  kusuasua zikiwemo hatua za kupunguza kodi zilizoafikiwa  baada ya uchaguzi wa shirikisho uliofanyika mwezi Septemba mwaka uliopita. Endapo muungano wa vyama vya mrengo wa shoto na  kati vitaibuka washindi,mageuzi katika sekta ya afya huenda yasifanyike kama ilivyoahidi serikali ya Angela Merkel  pamoja na  suala la kuyapunguza matumizi ya nishati ya nuklia.Kulingana na kura za  maoni,vyama hivyo viwili shirika vina kibarua kigumu cha  kuwashawishi  wapiga  kura kuwachagua katika jimbo hili la  magharibi la North-Rhein Westphalia. Uongozi wa jimbo la North-Rhein Westphalia  unavishirikisha vyama vya  mirengo ya kati na kulia,kama ilivyo katika  serikali  kuu ya  shirikisho na hali imekuwa hivyo tangu  miaka mitano  iliyopita.Ni  katika jimbo hilo kunapatikana  eneo la Ruhr lililo na viwanda ambavyo vinatatizika kiuchumi kwasababu ya hali mbaya ya  fedha.

Mikopo  kwa Ugiriki

Kwa upande mwengine Kansela

Koalitionsverhandlungen in Berlin / Merkel Wulff Westerwelle Rüttgers

Muungano wa mrengo wa kati-kulia:Kansela Angela Merkel,CDU; Christian Wulff, Waziri Mkuu wa jimbo la Niedersachsen, Guido Westerwelle kiongozi wa FDP,na Jürgen Ruettgers, Waziri Mkuu wa jimbo la Northrhein-Westphalia

Merkel amekosolewa na wanasiasa wa vyama vya upinzani kwasababu ya suala la kuipa  Ugiriki msaada hasa  baada ya kutoiidhinisha  mwanzoni kwasababu  ya mitazamo tofauti.Baada ya  kuiunga mkono hatua ya kuikopesha  Ugiriki,Bibi Merkel alisema wiki iliyopita kuwa mpango huo lazima ufanikiwe  la sivyo mataifa mengine ya Ulayahuenda yakatumbukia kwenye tatizo kama hilo. Siku ya  Ijumaa ,Chama cha upinzani cha kisoshalisti cha SPD kiliisusia kura ya kuupitisha uamuzi wa kuipa Ugiriki msaada.Hatua  hiyo huenda  ikawabadili mawazo wapiga kura hii leo.Bibi Merkel  kadhalika amewarai waangalizi wa masuala ya fedha kuwatuliza wawekezaji kwa lengo la  kuimaliza misukosuko katika masoko ya  hisa ya mataifa yanayotumia sarafu ya euro.Uamuzi huo kamwe haukuridhiwa na raia wengi wa  Ujerumani

Itakumbukwa kuwa miaka mitano iliyopita,chama kilichokuwa madarakani cha Kansela  wa Ujerumani wa zamani Gerhard Schroeder kilishindwa katika uchaguzi  wa  jimbo hili laNorth-Rhein Westphalia,hali iliyosababisha uchaguzi wa mapema kufanyika naye kuupoteza wadhifa huo.Hata  hivyo hali kama hiyo  haitarajiwi kushuhudiwa safari hii  ila  endapo Waziri Mkuu  wa chama cha CDU,Jürgen Rüttgers,atashindwa;siasa za Ujerumani huenda zikabadilika  kwa kiasi  kikubwa  na chama chake kikapoteza ushawishi wake.Katika muongo mmoja  uliopita,chama cha CDU kimekuwa na ushawishi mkubwa kisiasa nchini Ujerumani.Matokeo yoyote ambayo hayatavipa vyama shirika  vilivyo madarakani  vya CDU-FDP ushindi yatakuwa pigo kubwa  kwa Kansela Angela Merkel.

Vituo vya  kupigia  kura vinatarajiwa kufungwa mwendo wa  saa kumi na   moja  jioni na  matokeo  kutangazwa muda mfupi baada ya hapo. 

Kwa sasa   vyama  hivyo vina viti 37 kati  ya vyote 69 bungeni.Endapo  vyama hivyo  vitashindwa  katika uchaguzi huu wa leo,muunganohuo utapoteza  viti sita bungeni.Kwa  mujibu  wa sheria, ili kuwa na turufu sharti muungano  wowote ule upate viti visivyopungua 35 bungeni.Kwa mujibu wa ratiba,hakuna uchaguzi mwengine wa jimbo uliopangwa  kufanyika mwaka huu hapa Ujerumani.

Mwandishi:Thelma  Mwadzaya-RTRE/AFPE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

DW inapendekeza

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com