Trump kumkaribisha Putin Washington kwa mkutano wa pili | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.07.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump kumkaribisha Putin Washington kwa mkutano wa pili

Msemaji wa ikulu Sarah Sanders amesema Rais Trump amemtaka mshauri wake wa usalama wa taifa John Bolton kumualika Putin Washington

Rais wa Marekani Donald Trump ambaye anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kuhusu mkutano wake wa kilele na rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Helsinki wiki hii, amesema anakusudia kumualika Putin kwa mkutano mwingine tena mjini Washington baadaye mwaka huu na tayari mazungumzo yanaendelea.

Licha ya Rais Donald Trump kukumbwa na ukosoaji mkubwa baada ya mkutano wa kilele kati yake na Rais Vladimir Putin wiki hii kuhusu kile kilichotizamwa kuwa kuukubali msimamo wa Putin kwamba Urusi haikuingilia uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016, msimamo ambao ni kinyume na msimamo wa mashirika ya ujasusi ya Marekani, msemaji wa ikulu ya White House Sarah Sanders amesema kwenye ukurasa wa Twitter kuwa mkutano kati ya Trump na Putin huenda ukafanyika baadaye mwaka huu. Sanders ameandika kuwa Rais Trump amemtaka mshauri wake wa usalama wa taifa John Bolton kumualika Putin mjini Washington na tayari mazungumzo kuhusu mwaliko huo yameshaanza.

Mwaliko huo umekuja kama mshangao kwa mkurugenzi wa ujasusi wa Marekani Dan Coats alipoambiwa kuuhusu, wakati akihojiwa moja kwa moja katika kongamano la usalama la Aspen jimbo la Colorado. Akizungumzia mkutano uliopita kati ya Trump na Putin, Coats aliongeza kuwa:

Rais wa Marekani Donald Trump akizungumzia mkutano wake wa kilele na Rais wa urusi Vladimir Putin

Rais wa Marekani Donald Trump akizungumzia mkutano wake wa kilele na Rais wa urusi Vladimir Putin

"Sijui kilichojiri katika mkutano huo. Ninafikiri kadri muda unavyosonga na tayari rais amedokeza baadhi ya yale yaliyojiri. Ninafikiri tutafahamu mengi. Lakini hilo ni jukumu la rais. Lau angaliniuliza namna ylilipaswa a kulishughulikiwa, ningalimpendekezea njia tofauti. Lakini hilo si jukumu langu, wala kazi yangu, na ndivyo hali ilivyo."

Mapema siku ya Alhamisi, Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa anatarajia mkutano wao wa pili huku akitetea utenda kazi wake siku ya Jumatatu, ambapo yeye na Putin walizungumzia masuala mbalimbali ikiwemo ugaidi, usalama wa Israel, kuongezeka kwa silaha za nyuklia na Korea Kaskazini.

Lakini seneta wa chama cha Democratic Chuck Schumer amesema Trump hapaswi kukutana na Putin tena faraghani mahali popote hadi Wamarekani wajue yaliyojiri katika mkutano wao wa kwanza.

Ukosoaji mkali umemlazimisha Trump kujitetea, hali ambayo imemfanya yeye pamoja na ikulu ya Marekani kutoa kauli za kukanganya.

Trump amekanusha ukosoaji dhidi yake huku akisema kile alichokitaja kuwa vyombo vya habari za uwongo" kushindwa kutambua mafanikio yake.

Rais wa Urusi Vladimir Putin akisikiliza wakati Donald Trump akizungumza wakati wa mkutano wao wa kilele mjini Helsinki

Rais wa Urusi Vladimir Putin akisikiliza wakati Donald Trump akizungumza wakati wa mkutano wao wa kilele mjini Helsinki

Amesema mkutano wa kilele na Urusi ulikuwa wa mafanikio makubwa.

Katika tukio jingine, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema lengo kuu la Trump lilikuwa kuzielekeza upya nchi mbili ambazo zimekuwa zikifuata njia mbaya.

Pompeo aliliambia kituo cha televisheni cha Kikatoliki EWTN kwamba kumekuwa na joto jingi lakini mwanga kidogo tu kuhusu hotuba ya Trump kwa waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Putin. Ameongeza kuwa alitizama mahusiano kati ya Trump na Putin baada ya mkutano wao wa faragha na kwamba lengo la Trump lilikuwa kujenga njia ya mawasiliano na mazungumzo na alifaulu kwa hilo.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha CNBC, Trump alisema kuwa na mahusiano mema na Putin na Urusi kwa ujumla ni jambo chanya.

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo