TP Mazembe watwaa Super cup Afrika | Michezo | DW | 22.02.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

TP Mazembe watwaa Super cup Afrika

Cacau atamba kwa Stuttgart katika Bundesliga

Cacau atia mabao 4 pekee dhidi ya Cologne (5:1)

Cacau atia mabao 4 pekee dhidi ya Cologne (5:1)

TP Mazembe, ni timu ya kwanza kabisa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kutwaa Kombe la Super Cup la Afrika-Kura imepigwa kwa kinyan'ganyiro cha cha Kombe lijalo la bara la Afrika-Tanzania ikiangukia kundi la kufa-kupona-asema george Njongopa kutoka Dar-es-salaam-

Bayer Leverkusen, bado haikushindwa tangu mapambano 23 ya Bundesliga na iko bado kileleni.Mabao ya Muivory Coast,Didier Drogba yaipa Chelsea mwanya wa pointi 4 kileleni mwa Premier League.

TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, imekuwa timu ya kwanza mwishoni mwa wiki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kutwaa Kombe la Afrika la "Super Cup".TP Mazembe, iliitandika Stade Malien ya Mali mabao 2:0 jana mjini Lumbubashi na kuongeza taji hilo katika lile la klabu bingwa ililolitwa mwishoni mwa mwaka uliopita.

Lakini, hawakuwa wakongamani waliotikisa wavu bali mabao yote 2 ya TP Mazembe yalitiwa na wazambia:Stopila Sunza alilifumania lango la Stade Malien tayari mnamo dakika ya 15 ya mchezo kabla mshambulizi Singuluma,akiupiga msumari wa mwisho katika jeneza la Stade Malien dakika 10 kabla ya firimbi ya mwisho kulia.

Ushindi wa Mazembe tangu wa taji la Champions league na hata dhidi ya mabingwa Stade Malien, kumekomesha mamlaka ya timu za Afrika ya kaskazini ya kombe hili la Super cup:Kwani, Al Ahly ya Misri, ilinyakua mataji 3 kati ya 4 na Etoile du Sahel ikatwaa taji la 4.

Afrika Kusini, wenyeji wa Kombe lijalo la dunia hapo Juni 11-hadi Julai 11, mwaka huu na moja kati ya timu 6 za Afrika,imebadili kambi yake ya mazowezi na hii ni miezi 4 tu kabla ya Kombe la dunia.Afrika kusini hairidhiki na kambi yake ya sasa.Bafana bafana, haitaki kutumia shule ya Esselen Park School iliopo karibu na jiji la Johannesberg.Badala yake ,Bafana bafana, itaopiga kambi yake katika Sandown High School,iliopo kiasi cha km 40 kutoka Johannesberg.

Kura ilipigwa Jumamosi ya kinyan'ganyiro cha Kombe la Afrika la Mataifa 2012. Eric Ponda na George Njongopa, wanasimulia kutoka Mombasa na Dar-es-salaam jinsi Harambee Stars na Taifa Stars zimeangukia makundi gani.Njogopa adai Tanzania haitapona mbele ya madume wa Afrika ya kaskazini:

Ama katika Bundesliga na Premier League: Bayer Leverkusen imeun'gan'gania usukani wa Bundesliga wakati Chelsea ule wa Premier League baada ya Manchester United kuteleza.Bao la dakika ya mwisho la Werder Bremen, liliwanyima viongozi wa Bundesliga, Bayer Leverkusen pointi 3 wakati ikidhani imeshazitia mfukoni.

Mlinzi wa Bremen na timu ya Taifa, Per Mertesacker,alitia bao la kusawazisha na kufanya matokeo 2:2 mnamo dakika ya 93 ya kufidia mchezo.Laiti Leverkusen, ingeondoka na ushindi huko Bremen, basi ingelifungua mwanya wa pointi 2 kileleni kati yake na Bayern Munich ambayo iliteleza mwishoni mwa wiki ilipotoka sare bao 1:1 na jirani zao wa kusini, Nüremberg.Kocha wa Bayer Leverkusen,Jupp Hynckes, akihuzunika kwa kupoteza pointi 3 kwa sare hiyo ya 2:2 na Bremen alisema,

"Bila ya shaka inahuzunisha sana kwa kutiwa bao dakika ya 93 ya mchezona adui kusawazisha.Hatahivyo, haidhuru si vibaya,kwani timu yangu imeonesha kutoridhika na sare ya mabao 2:2 na Bremen na hii yaonesha jinsi ilivyovinjari kucheza bora zaidi."

Katika mpambano wa kusisimua kabisa wa Bundesliga, mwishoni mwa wiki, Stuttgart iliichezesha FC Cologne ,kindumbwe-ndumbwe na kuiabisha nyumbani mwake kwa mabao 5:1.Mbrazil aliechukua uraia wa Ujerunmani,Cacau, ndie jogoo hasa wa Stuttgart aliewika siku hiyo.Cacau alitia mabao 4 pekee katika lango la Cologne.Mwishoni mwa mpambano huo,mbrazil huyo aliechukua uraia wa Ujerumani na yumo katika kikosi cha Taifa,alitoa salamu zake kwa kocha wa Ujerumani aliposema:

"Si uzuri kutocheza dimba kwa muda mrefu.Ndio maana, nimeufarahia sana mpambano huu na halfu kuja kutia mabao 4 na timu yetu kutamba na kushinda, ni jambo linalofurahisha zaidi."Alisema Cacau akitumai kwa mabao yake hayo 4 kocha waTaifa, Joachim Loew, atamwita kujiunga na kikosi chake kwa Kombe lijalo la dunia.

Mpambano mwengine wa kusisimua mabingwa watetezi Wolfsburg, waltoka nyuma na kuikandika Schalke iliopo nafasi ya 3 ya ngazi ya Ligi,mabao 2:1.Alikuwa Mbrazil mwengine,Grafite, aliefuta bao la Kevin Kuranyi mnamo dakika ya 71 ya mchezo kabla hajarudi dakika 6 baadae kwa bao lake la pili.Hertha Berlin, inayoburura mkia muda mrefu ilitichapa Freiburg mabao 3:0 na sasa inaweka matumaini ya kubakia katika Bundesliga.

Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,Cheksea imefungua mwanya wa pointi 4 mbele ya mahasimu wao Manchester united.Mabao 2 ya Muivory Coast, Didier Drogba, yalichangia ushindi wa mabao 3-1 wa Chelsea dhidi ya Wolvehapton Wanderes .Manchester United, iliteleza ilipokomewa mabao 3:1 na Everton.

Mwandishi:Ramadhan Ali /AFPE/DPA

Uhariri: M.Abdulrahman