1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tofauti bado ipo kati ya EU na Trump kuhusu Urusi

25 Mei 2017

Rais wa Marekani Donald Trump Alhamis alikumbana na matatizo ya kwanza katika ziara yake ya Ulaya, baada ya kushutumiwa hadharani kuhusiana na uhusiano wake na Urusi.

https://p.dw.com/p/2dZej
Brüssel EU Gipfel Brexit Verhandlungen Tusk
Donald Tusk rais wa Baraza la Umoja la UlayaPicha: picture-alliance/dpa/M. Meissner

Trump pia ameshutumiwa kwa uvujishaji wa taarifa za kijasusi kuhusiana na lile shambulizi la kigaidi la Manchester. Ziara yake ya kukutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya kujihami ya NATO, ilikuwa ni ya kuupunguza mgawanyiko uliotokana na matamshi yake makali dhidi ya taasisi hizo mbili  wakati wa kampeni za uchaguzi huko Marekani.

Kulizuka tofauti mara baada ya mazungumzo yake na maafisa wakuu wa Umoja wa Ulaya, Donald Tusk ambaye ni rais wa baraza la Umoja huo na mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, kuhusiana na masuala ya tabia nchi, biashara na zaidi ya yote Urusi.

"Kivyangu nahisi tumekubaliana mengi, kwanza kabisa kuhusiana na kukabiliana na ugaidi na nina uhakika sistahili kuelezea kwanini. Lakini hakukuwa na mwafaka katika masuala mengine kama tabia nchi na biashara," alisema Tusk. "Lakini sina uhakika wa asilimia mia moja kwamba sisi tuanweza kusema leo, na nikisema sisi namaanisha rais Trump na mimi mwenyewe, kwamba tuna msimamo na mtazamo mmoja kuhusiana na Urusi."

Trump amelegeza msimamo wake kuhusu Brexit

Wakati wa kampeni Trump aliahidi kurejesha uhusiano mzuri baina ya Marekani na Urusi lakini amekabiliwa na upinzani mkali huko Marekani na amekabiliwa na sakata ya kutoa taarifa muhimu kwa Urusi. Rais huyo wa Marekani pia aliushangaza Umoja wa Ulaya kwa kuunga mkono kujiondoa kwa Uingereza katika Umoja huo Brexit, huku akiutaja kama chombo cha Ujerumani kuitawala Ulaya.

Lakini duru kutoka Umoja wa Ulaya zinasema Trump alimwambia Tusk na Juncker kwamba sasa ana hofu ya Wamarekani kupoteza kazi kutokana na brexit mwaka 2019.

Belgien Donald Tusk und Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump akiwa BrusselsPicha: Reuters/F. Lenoir

Akiwasili mjini Brussels Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May aliahidi kuzungumzia masuala kadhaa katika huo mkutano wa NATO, akisema atazungumza waziwazi kuhusiana na suala la utoaji wa taarifa za kijasusi baina ya mashirika ya usalama.

"Katika suala la kubadilishana taarifa za kijasusi na Marekani, tuna uhusiano mzuri sana na Marekani lakini uhusiano huo umejengwa kwa msingi wa uaminifu," alisema May, "na uaminifu huo ni kuhakikisha kwamba taarifa zinaweza kutolewa  bila wasiwasi, na nitaweka wazi mbele ya rais Trump leo kwamba ni sharti kuwe na usalama kwa taarifa za kijasusi zinazotolewa."

May atamwambia Trump waziwazi kuwe na usalama katika utoaji taarifa za kijasusi

Kauli hii ya May imekuja wakati ambapo kuna taarifa zinazosema kwamba Marekani ilivujisha taarifa za kijasusi kuhusiana na lile shambulizi la Manchester, jambo lililoughadhabisha uongozi wa Uingereza.

Die Britische Premierministerin Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May Picha: Imago/Zumapress/T. Akmen

Lakini Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau yeye alisema nchi yake itaendelea kutoa taarifa za kijasusi kwa Marekani kama ilivyokuwa ikifanya hapo awali na pia itajitolea kuunga mkono azimio la NATO.

"NATO inawakilisha demokrasia na sheria ambayo ni mambo yanayotuunganisha, pamoja na ushirikiano wetu wa kimataifa na wale wanaohitaji msaada wetu," alisema Trudeau, "na Canada itaendelea kutoa ushirikiano sasa na katika siku za mbeleni. Natazamia kwamba tutakuwa na mkutano mzuri leo pamoja na nchi zengine wanachama wa NATO."

Kuijumuisha jamii ya NATO katika ule muungano unaoongozwa na Marekani katika kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu ndiyo lengo kuu la rais Trump huko Brussels na mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema jamii hiyo itakubali kujiunga na muungano huo wa kijeshi wa Marekani katika mkutano huo.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu