1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tahrir ya Misri yavuma tena

29 Juni 2011

Polisi nchini Misri wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji katika uwanja wa Tahrir, wanaolalamika kwamba mchakato wa hatua za kisheria kwa maafisa wa zamani wa nchi hiyo umekuwa wa kusuasua.

https://p.dw.com/p/11lQb
Waandamanaji nchini Misri wakikabiliana na polisiPicha: picture-alliance/dpa

Vurugu hizo zilianza jana jioni, katika eneo ambalo zaidi ya watu 840 waliuawa katika vuguvugu la upinzani mwezi Februari lililomuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak.

Katika eneo hilo maarufu kama uwanja wa Tahrir, waandamanaji walikusanyika kwa shabaha ya kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Misri kiasi ya polisi 41 na raia wawili wamejeruhiwa katika purukushani hizo. Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo imesema mpaka sasa polisi inawashikilia watu saba kwa tuhuma ya kuchochea maandamano.

Ägypten Hosni Mubarak
Rais wa zamani wa Misri, Hosni MubarakPicha: AP

Hii na mara ya kwanza kutokea kwa vurugu kama katika uwanja wa Tahrir baada ya wiki kadhaa zilizo sababisha kumuondoa madarakani Mubarak. Polisi walivaa mavazi ya kujikinga wasidhurike wakiwa na ngao waliwazuia waandamanaji waliokusanyika mbele ya wizara.

Wahudumu katika gari za kubebea wagonjwa walionekana wakiwatibu watu watu walioathirika na mabomu ya kutoa machozi. Mwandishi wa Shirika la Habari la Ufaransa alishuhudia baadhi ya watu wakiwa na majeraha madogo madogo, wakiwemo walioumia kichwani.

Ahmed Abdel Hamid mwenye umri wa miaka 26, ni mwajiriwa katika kiwanda cha kuoka mikate akiwa katika uwanja wa mapambano alisema watu wana hasira kutokana na kucheleweshwa kwa kesi za waliokuwa maafisia wa ngazi za juu wa nchi hiyo.

Baadhi wa waandamanaji wametoa wito wa kumtaka Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Misri, Mohammed Hussein Tantawi ajiuzulu.

Sefie Helden ni Afisa wa Polisi wa Zamani alisema" Sijaona polisi wakitumia nguvu kupita kiasi, nilichoona polisi walikuwa wakijaribu kuyalinda baadhi ya majengo muhimu ambayo yapo karibu na uwanja wa Tahrir, kama Chuo Kikuu Cha Kimarekani, majengo kadhaa kama ya kibalozi na makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani"

Lakini Baraza la Kijeshi katika kauli yake iliyosambazwa katika mtandao wa facebook mkusanyiko huo hauna maana yeyote zaidi ya kuhatarisha usalama wa nchi hiyo.

Hivi karibuni waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani wa Misri, Habib al-Adli amehukumuiwa kifongo kwa tuhuma za rushwa lakini kiongozi huyo wa zamani na maafisa wengine kadhaa wanakabiliwa na mashitaka yanayohusiana na mauwaji ya waandamanaji.

Katika vuguvugu la upinzani lasiku 18 lililomuondoa madarakani rais Hosni Mubarak polisi walitumia, mabomu ya kutoa machozi na silaha nyingine za moto. Na rais huyo wa zamani kwa sasa yupo hospitali akiugua saratani.

Kesi ya Mubarak anayetuhumiwa pia kwa mauaji ya waandamanaji na anaweza kukabiliwa na adhabu ya kifo endapo atakutwa na hatia. Kesi yake inatarajiwa kusikilizwa Agosti 3.

Mwandishi: Sudi Mnette/RTR

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed