Shehena ya silaha ya meli iliotekwa nyara ni ya Sudan kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Shehena ya silaha ya meli iliotekwa nyara ni ya Sudan kusini

Maharamia wa Somali wanaoishikilia meli ya Ukraine yenye shehena ya kijeshi wamesema leo hii kwamba silaha ilizobeba zilikuwa zinaelekea Sudan na sio Kenya.

default

Fukwe za Somalia pichani ni mojawapo ya fukwe hatari kabisa duniani kutokana na vitendo vya kiharamia.

Maharamia hao pia wamekanusha kwamba wenzao watatu wameuwawa katika mashambuliano ya risasi baina ya maharamia hao.

Habari za shehena hiyo ya silaha zimekuwa zikitatanisha baada ya Kenya kusema kwamba zilikuwa zinaelekea nchini mwake.

Msemaji wa maharamia hao Sungule Ali amekaririwa akisema kwa njia ya simu ya sataliti kutoka kwenye meli hiyo walioiteka nyara kwamba wanathibitisha kwamba silaha hizo hazimilikiwi na serikali ya Kenya bali na Sudan kusini.

Akigusia juu ya madai yao ya kupatiwa fedha za kuigombowa meli hiyo amesema kwamba hawajali silaha hizo zinamilikiwa na nani kwani hilo sio tatizo lao bali tatizo lao ni dola milioni 20.

Nathan Christensen msemaji wa Kikosi cha Tano cha Manowari za Marekani kilioko nchini Bahrain amesema hapo jana kwamba meli hiyo MV Faina na shehena yake ya vifaru 33 vya kivita vya Kirusi na zana nyengine za kijeshi zilikuwa zimeazimiwa kupelekewa mteja alieko Sudan kusini.

Serikali ya Kenya na ile ya Ukraine pamoja na msemaji wa jeshi la Sudan wote wameyakataa madai hayo ya serikali ya Marekani.

Meli hiyo iliotekwa nyara na maharamia wa Somalia katika bahari ya Hindi mwishoni mwa juma lililopita wakati ikiwa njiani kuelekea katika bandari ya Mombassa nchini Kenya nyendo zake hivi sasa zimekuwa zikifuatliwa na manowari za kivita za Marekani.

Kenya imesema tokea mwanzo kabisa kwamba shehena hiyo ya silaha ilikuwa ikiwasilishwa kama sehemu ya makubaliano na Ukraine kuzifanya zana zake za kijeshi kuwa za kisasa.

Maharamia hao wamekuwa wakidai mamilioni ya dola kuiachilia huru meli hiyo ilioandikishwa Belize,shehena yake na mabaharia 21 wakiwemo Waukraine, Warusi na Walatvia.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Urusi nahodha wa meli hiyo amefariki kutokana na kuuguwa ndani ya meli hiyo.

Sugule msemaji wa maharamia amesema wanaendelea kushikilia madai yao ya kupatiwa dola milioni 20 na kwamba hizo sio fedha za kuigombowa meli hiyo bali ni faini kwa kusafirisha silaha kinyume na sheria katika bahari ya Somalia.

Msemaji huyo amekanusha madai ya Andrew Mwangura mkuu wa shirika linaloshughulikia usalama wa mabaharia kanda ya Afrika Mashariki kwamba maharamia watatu wameuwawa katika mashambuliano ya risasi yaliochochewa na kutofautiana juu ya nini cha kufanya kwa meli hiyo walioiteka.

Amesema hiyo ni propaganda inayoenezwa na baadhi ya watu wasiojuwa juu ya hali waliyo nayo maharamia hao na kwamba wao wako kitu kimoja na wanawaadhibu wale wanaotumia vibaya bahari ya Somalia.

Mwangura alisema maharamia wa msimamo wa wastani na wale wa msimamo mkali walipambana hapo jana.

Uharamia kwenye fukwe za Somalia zisizokuwa na doria katika Bahari ya Hindi na Ghuba ya Aden umeanza miaka mingi iliopita kama juhudi za kuzuwiya mashua za uvuvi za kigeni zinazotumia karibu na kumaliza kabisa mali asili ya baharini ya nchi hiyo.

 • Tarehe 30.09.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FRbG
 • Tarehe 30.09.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FRbG
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com