1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Ujerumani kutekeleza makubaliano yake na Namibia

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
2 Septemba 2022

Serikali ya Ujerumani licha ya lawama zinazotolewa imesema inakusudia kuyatekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Namibia juu ya mauaji ya kimbari ya wahereo.

https://p.dw.com/p/4GMZH
Namibia Geschichte Deutsch-Südwestafrika Gefangene Hereros
Picha: ullstein bild

Pana ukimya juu ya maridhiano yaliyofikiwa kati ya Ujerumani na Namibia. Tangu mwaka uliopita tamko la pamoja juu ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Wajerumani nchini Namibia lipo mezani. Hata hivyo serikali za Ujerumani na Namibia bado hazijatia saini. Wapinzani nchini Namibia pamoja na ndugu wa wahanga wa mauaji wanataka mazungumzo yafanyike upya.

Kina mama wa kabila la Waherero nchini Namibia.
Kina mama wa kabila la Waherero nchini Namibia.Picha: AP

Hata hivyo baada ya kunyamaza kimya kwa muda mrefu serikali ya Ujerumani imelikataa pendekezo hilo. Ujerumani imeeleza kuwa tamko hilo la pamoja limeshazungumziwa na kukamilishwa. Serikali ya Ujerumani imeeleza hayo ilipojibu swali la mbunge wa chama cha mrengo wa shoto Sevim Dagdelen aliyesema: ''Hatua hii inaonesha kiburi cha serikali. Malalamiko makubwa ya wabunge wa Namibia na ghadhabu za ndugu wa wahanga wa uhalifu wa wajerumani wakati wa ukoloni vinapuuzwa na serikali ya Ujerumani na badala yake Namibia ndiyo inayolaumiwa.''

Serikali ya Ujerumani haitaki kulipa fidia bali inataka kuzuia malipo kwa ajili hiyo inatumia nguvu zake kubwa za kisiasa dhidi ya Nambia. Watu wa makabila ya waherero na wanama pia wana mtazamo kama huo. Watu hao waliomba kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani mnamo mwezi Desemba mwaka jana.

Zed Ngavirue, Mwakilishi Mkuu wa Serikali ya Namibia kwenye mazungumzo na Ujerumani.
Zed Ngavirue, Mwakilishi Mkuu wa Serikali ya Namibia kwenye mazungumzo na Ujerumani.Picha: Adrian Kriesch/DW

Waherero na wanama wanapinga tamko la pamoja linalotambua tu wajibu wa kiuadilifu wa Ujerumani juu ya mauaji lakini siyo wajibu wa kisheria. Watu wa Namibia pia wanapinga pendekezo la msaada wa dola bilioni moja utakaotolewa kwa kipindi cha miaka 30. Mwanaharakati wa Nambia Sima Luipert amesema huo ni ushirikiano wa kuleta maendeleo na yanayohusika hapa ni ufadhili wa miradi ya miundombinu. Amesema hilo ni jambo zuri, lalkini hisani hiyo haitatui suala la msingi. Wanaharakati wa waherero wanapinga. Mjumbe wao Ueiruka Tjikuua amesema wanaofanya mazungumzo na serikali ya Ujerumani wanapaswa kuwawakilisha watu wote wa Namibia.

Wakati huo huo serikali ya Ujerumani inajitayarisha kutoa awamu ya kwanza ya fedha za msaada. Kiasi cha Euro milioni 35  kimepangwa kutolewa mnamo mwaka huu kwa ajili ya miradi kadhaa ya maendeleo. Sehemu ya fedha hizo pia zitatolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kumbukumbu ya mauaji ya wanama na waherero yaliyofanywa na wajerumani wakati wa ukoloni.

Bunge la Namibia
Bunge la NamibiaPicha: imageBROKER/picture alliance

Fedha hizo ni sehemu ya msaada wa maendeleo wa  jumla ya Euro bilioni moja uliopagwa kutolewa katika muda wa miaka 30. Hata hivyo bado haijajulikana ni wakati gani miradi hiyo itaanza kutekelezwa. Lakini pia ni muhimu kutambua kwamba watu wa Namibia bado wana mashaka juu ya tamko la pamoja linalohusu mauaji ya halaiaki yaliyofanywa na wajerumani nchini Namibia wakati wa ukoloni.