1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Tanzania yawasaka wakimbizi wasio na vibali

9 Aprili 2026

Serikali mkoani Kigoma magharibi mwa Tanzania, imeamuru kuanza msako dhidi ya wahamiaji wasio na vibali pamoja na wakimbizi wanaotajwa kutoroka kambi katika mkoa huo, huku wananchi wakihimizwa kushiriki msako huo.

https://p.dw.com/p/5BuEd
Wakimbizi wa Kongo nchini Tanzania
Wakimbizi wa DRC wakisajiliwa nchini TanzaniaPicha: Prosper Kwigize/DW

Kufuatia msimamo wa serikali ya Tanzana kufunga kambi na kufanya msako wa wahamiaji, baadhi ya wananchi mkoani Kigoma wameonesha kuwepo kwa uhitaji wa raia wa kigeni katika kutekeleza shughuli za kiuchumi na kutoa wito wa wahamiaji au wakimbizi kupata vibali ili kuishi kwa amani

Wakizungumza na DW wananchi hao wamesema kuwepo kwa wahamiaji wasio na vibali kunaweza kuwa hatari kwa usalama. Juma Kimtanange mkazi wa Kigoma pamoja na kuungam kono msako dhidi ya wakimbizi anasema.

"Kisheria ukimchukua lazima ufate sheria, uwe na vibali kutoka migration, au kutoka kwenye taasisi husika, sasa wewe unawachukua maana yake hata ikitokea uhalifu na wewe utakuwa mmojawapo wa wahalifu, kwa hiyo ushauri wangu wanaowachukua bila vibali wafuate sheria."

Tanzania Burundi-Wakimbizi
Mkimbizi wa Burundi Nzeyimana Consolate akiwa amembeba mtoto wake katika eneo la Nyabitara Transit, akiwa ni miongoni mwa wakimbizi wa Burundi waliorejea nchini mwao kutokea Tanzania 2019 hPicha: Tchandrou Nitaga/AFP/Getty Images

Akizungumza na DW kwa njia wa simu Mkuu wa Uhamiaji mkoa wa Kigoma Kamishna msaidizi mwandamizi Dismas Lucian Mlula amebainisha kuwa tayari zaidi ya wahamiaji 200 wamekamatwa katika msako huo uliotangazwa na mkuu wa mkoa wa Kigoma ambao hadi sasa unaendelea.

"Zaidi ya 200 mpaka dakika hii kwasababu waliondoshwa wako zaidi ya 200; baada ya kuona uhamiaji haramu namna walivyotapakaa kwenye maeneo mbalimbali, lakini kutokana na uondoshwaji wa wakimbizi, baadhi wanaondoka wengine wanarejea, lakini wengine wanaonekana kutoridhia Kwenda, wahamiaji haramu wako maeneo mengin nchini lakini lango ni Kigoma."

Mlula ameeleza kuwa kumekuwepo na wimbi la raia wa kigeni hasa kutoka Burundi na Rwanda wanaoingia kuishi na kufanya kazi bila vibali, akitoa wito kwa rai awa nchi jirani kufuata taratibu.

Wakimbizi waishio Tanzania watakiwa kurejea Burundi

Awali Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Inspekta Jenerali mstaafu wa Polisi Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha wakuu vwa vitengo vya ulinzi na usalama mkoani humo alielekeza kusakwa kwa wahamiaji kila eneo.

"Taarifa tulizopata ni kwamba baadhi ya waliokuwa kambi ya nduta hawataki kurudi kwao, wakati makubaliano na serikali yao ni kwamba hakuna matishio na wengi wameanza kurudi kwao na wengine wanagoma na kutoroka kambini na kuanza kuingia kwenye maeneo yetu ya mkoa wa Kigoma", alisema Sirro. 

Tanzania imezaimia kufunga kambi zote zinazohifadhi wakimbizi wa Burundi na kuhakikisha wote wanarejea ingawa zoezi hilo linakabiliwa na upinzani kutoka kwa wakimbizi wengi wakionesha kutokuwa tayari kurejea Burundi kwa sasa