1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afya ya Kizza Besigye yazidi yadorora gerezani Uganda

20 Januari 2026

Chama cha upinzani nchini Uganda cha People's Front for Freedom, kinasema afya ya Kizza Besigye, aliyefungwa gerezani, imefikia hali mbaya. Serikali na magereza wamekana madai hayo huku wafuasi wakihofia maisha yake.

https://p.dw.com/p/5771I
Uganda Kizza Besigye Oppositionspolitiker
Picha: BADRU KATUMBA/AFP

Afya ya mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, inaelezwa kuzidi kudhoofika akiwa gerezani, kulingana na chama chake. Taarifa hiyo imesababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa wafuasi wake na wanaharakati wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa chama cha People's Front for Freedom, Besigye alisafirishwa usiku kucha hadi katika kituo cha matibabu mjini Kampala. Chama hicho kimesema hali yake "imefikia kiwango cha hatari na inaendelea kuzorota.”

Katika taarifa yake, chama hicho kilidai Besigye ananyimwa haki ya msingi ya kupata matibabu yenye hadhi. Kilitaka madaktari wake binafsi na familia yake waruhusiwe kumuona bila vizuizi.

Besigye anazuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali jijini Kampala. Anakabiliwa na mashtaka ya uhaini, ambayo yeye na wafuasi wake wanayatafsiri kama njama ya kisiasa.

Uganda | Kizza Besigye mahakamani
Besigye anashtumiwa na utawala wa Rais Yoweri Museveni kwa kupanga njama ya mapinduzi.Picha: Hajarah Nalwadda/AP/picture alliance

"Ni jambo la kusikitisha kuona mtu aliyetoa maisha yake kwa uhuru wa wengine akinyimwa haki zake,” ilisema taarifa ya chama hicho. Serikali na mamlaka za magereza zilitajwa kuwajibika kikamilifu kwa usalama wake.

Magereza wakanusha Besigye kuwa na hali mbaya

Hata hivyo, mamlaka za magereza ya Uganda zimepinga madai hayo. Msemaji wa magereza, Frank Baine, alisema Besigye alifanyiwa uchunguzi wa kawaida tu.

Alisema safari ya Besigye kwenda hospitalini haikuwa ya dharura. "Asubuhi alikuwa anaendelea na mazoezi yake,” Baine aliongeza.

Besigye ni mmoja wa sura kuu za upinzani wa Uganda kwa miongo kadhaa. Aligombea urais mara kadhaa na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2016.

Baada ya uchaguzi huo, Besigye alisema kushiriki uchaguzi nchini Uganda ni kupoteza muda. Alidai mamlaka ya rais yanategemea zaidi jeshi kuliko ridhaa ya wananchi.

Tangu wakati huo, amekuwa akihamasisha aina nyingine za upinzani nje ya sanduku la kura. Hatua hizo zimemweka mara kwa mara katika mgongano na vyombo vya dola.

Besigye afikishwa mahakama ya kijeshi

Uchaguzi uliogubikwa na madai ya udanganyifu

Wakati huo huo, Uganda imemaliza uchaguzi mwingine wa urais. Rais Yoweri Museveni alitangazwa mshindi kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura.

Mpinzani wake mkuu, Bobi Wine, alikataa matokeo hayo. Alisema uchaguzi huo ulikuwa na dosari kubwa na haukuwa wa haki.

Uchaguzi huo ulikumbwa na kukatika kwa mtandao wa intaneti kwa siku kadhaa. Pia kulikuwa na hitilafu za mashine za uthibitishaji wa wapiga kura.

Wanaharakati wa demokrasia wanasema mashine hizo zilikuwa muhimu kudhibiti wizi wa kura. Serikali ilikanusha madai ya udanganyifu.

Museveni, mwenye umri wa miaka 81, amekuwa madarakani tangu mwaka 1986. Kwa miaka mingi amebadili katiba ili kuendelea kushika hatamu za uongozi.

Harakati za mapambano za Besigye

Ukomo wa mihula na masharti ya umri yaliondolewa kwenye katiba. Hatua hiyo ilifungua njia kwa Museveni kuendelea kugombea bila vikwazo vya kisheria.

Baadhi ya wapinzani wake wamefungwa au kutengwa kisiasa. Wengine wamelazimika kuishi uhamishoni.

Besigye ni daktari kwa taaluma na kanali mstaafu wa jeshi. Awali alikuwa mshirika wa karibu wa Museveni, akihudumu kama msaidizi wake wa kijeshi na daktari binafsi.

Besigye apandishwa tena kizimbani

Baadaye, aligeuka kuwa mkosoaji wake mkali zaidi. Aliwahi kuongoza chama cha Forum for Democratic Change, chama kikuu cha upinzani kwa miaka mingi.

Besigye amekuwa kizuizini tangu Novemba 2024. Anadaiwa kupanga njama za kuipindua serikali, madai ambayo anakanusha vikali.

Shutuma za Muhoozi dhidi ya Besigye

Mtoto wa Rais Museveni, Mkuu wa Majeshi Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amemshutumu Besigye hadharani. Amewahi kudai kuwa Besigye alipanga kumuua baba yake.

Kauli hizo zimekosolewa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu. Wanasema zinachochea chuki na kuhatarisha usalama wa Besigye.

Museveni mwenyewe amesema Besigye lazima awajibike kwa "makosa mazito” anayodaiwa kupanga. Ameitaka kesi yake isikilizwe haraka.

Wafuasi wa Besigye wanasema mashtaka hayo yana lengo la kumtoa kwenye mchakato wa kisiasa wa baada ya Museveni. Wanasema ni njia ya kuzima upinzani.

Wachambuzi wengi wanaona Uganda ikielekea kipindi kisicho na uhakika wa kisiasa. Museveni hana mrithi wa wazi ndani ya chama tawala cha NRM.