1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanawe rais wa Uganda amtishia kiongozi wa upinzani

20 Januari 2026

Mkuu wa majeshi ya Uganda Muhoozi Kainerugaba, amesema anataka kuona kiongozi wa upinzani Bobi Wine akiwa amekufa, siku chache baada ya Wine kudai kuwa alilazimika kujificha.

https://p.dw.com/p/576qn
Uganda Entebbe 2024 | Maadhimisho ya miaka 50 ya kuzaliwa kwa Muhoozi Kainerugaba
Mkuu wa majeshi ya Uganda Muhoozi KainerugabaPicha: Ugandan Presidential Press Unit

Katika ujumbe aliochapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X jana usiku, Kainerugaba amesema wamewauwa magaidi 22 wa chama cha NUP tangu wiki iliyopita na kwamba anaomba gaidi wa 23 awe Kabobi, akimzungumzia Wine na chama chake cha National Unity Platform (NUP).

Katika chapisho lingine, amesema amempa Wine muda wa saa 48 kujisalimisha kwa polisi la sivyo watamchukulia kama muasi na kumshughulikia ipasavyo.

Wine amekosoa vitisho hivyo vya Kainerugaba na kuwataka wanajeshi kuondoka kwenye nyumba yake, na akaongeza kuwa mke na watu wake hawako salama.

Bado hakuna maelezo kuhusu aliko Wine baada ya kusema Jumamosi kuwa alitoroka uvamizi wa polisi nyumbani kwake ambapo mkewe bado yuko chini ya kifungo cha nyumbani.