1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Haki za binadamuAfrika Kusini

Mashambulizi dhidi ya wageni kuongezeka Afrika Kusini?

6 Novemba 2023

Chuki dhidi ya wageni sio kitu kipya nchini Afrika Kusini, lakini wataalamu wanaonya kwamba mashambulizi dhidi ya wageni yanaweza kuongezeka wakati kampeni za kizalendo nazo zikizidi kushika kasi.

https://p.dw.com/p/4YSlt
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: Sergei Bobylev/imago images/ITAR-TASS

Chuki dhidi ya wageni sio kitu kipya nchini Afrika Kusini, lakini wataalamu wanaonya kwamba mashambulizi dhidi ya wageni yanaweza kuongezeka wakati kampeni za kizalendo nazo zikizidi kushika kasi. 

Jeshi lililojiteua la kiraia lililokuwa likishika doria mitaani katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini lilikuwa na lengo moja tu la "Kuwafukuza wageni".

Kundi la wanaounga mkono kikundi kikachopinga wahamiaji cha Operesheni Dudula lilivamia maduka ya wageni yanayojulikana kama "Spaza"  katika kijiji cha Diepkloof, ambako waliwanyanyasa wamiliki, wakikagua tarehe za mauzo ya bidhaa zao na hata kutishia kufunga maduka hayo.

Victress Mathuthu, raia wa Zimbabwe, alikuwa mmoja wa wale waliolengwa na raia wa Afrika Kusini ambao pia ni weusi na wanaowachukia wageni.

Amesema "Iwapo wafuasi wa Operesheni Dudula hawajaridhishwa na raia wa kigeni kupewa leseni za biashara ndogo ndogo, wanapaswa kuiambia serikali ama wizara husika.

Soma pia:Maoni: Vurugu Afrika Kusini zaharibu ndoto ya Afrika

Wanaounga mkono Operesheni Dudula hata hivzo wamedai kwamba wizara husika hazichukui hatua za kutosha za kuwazuia wageni kumiliki biashara na hivzo kujihahalishia kuchukua sheria mkononi.

Mratibu wa kitaifa wa Dudula Thabo Ngayo amesema "Hawaruhusiwi kumiliki duka la Spaza". Amesema hayo katika moja ya operesheni zao za ulinzi.

Alimwambia mmoja ya wamiliki hao wa kigeni ya kwamba biashara hizo zimetengwa kwa ajili ya Waafrika Kusini pekeena kwa maana hiyo duka kama hilo la Spaza lazima liwe la Mwafrika Kusini.

Hakuishia hapo, bali akasema "wana siku chache za kuondoka kwenye eneo hilo."

Mzwanele Manyi, ambaye ni mwakilishi wa chama cha Economic Freedom Fighters, EFF anakubaliana na hayo.

Yeye pia anatoa mwito wa kufungwa wa maduka hayo ya Spaza nchini Afrika Kusini. Ameaimbia DW kwamba hawawezi kuendelea kuvumilia hali kama hiyo.

Oparesheni Dudula yachochea ubaguzi?

Ubaguzi dhidi ya wageni sio kitu kipya nchinI Afrika Kusini. Mwezi Aprili, 2022, raia wa Zimbabwe aliyekuwa akiishi Diepsloot, kaskazini mwa Johannesburg, alipigwa mawe na kuchomwa moto.

Waafrika Kusini wanaounga mkono chuki dhidi ya wageni wakiandamana
Waafrika Kusini wanaounga mkono chuki dhidi ya wageni wakiandamanaPicha: Milton Maluleque/DW

Mwaka 2008, Waafrika Kusini walichoma moto mali za wageni katika maeneo yao na kuwaua watu 62.

Ghadhabu iliongezeka na mawimbi ya mauaji ya chukiyalisambaa, na hata uchunguzi ulioanzishwa wakati huo haukufika popote.

Kulingana na Kituo cha masuala ya Uhamiaji cha African Center for Migration and Society, ACMS katika chuo kikuu cha Witwatersrand, kulikuwa na mashambulizi 1,038 dhidi ya wahamiaji, vifo 661 na visa 5,131 vya uporaji kwenye maduka. 

Kundi la Operesheni Dudula kwa mara ya kwanza lilijitokeza kwenye mitandao ya kijamii mwaka 2020. Dudula ni neno la kabila ya Zulu linalomaanisha "kuwaondosha".

Kundi hilo hivi sasa limejisajili kama chama cha siasa na kitashiriki kwenye uchaguzi mkuu wa 2024.

Soma pia:Nigeria yamwita balozi wa Afrika Kusini kuhusu mashambulizi

Na sio tu mgombea wa Dudula atakayekuwa akipigia kelele suala hili, bali pia mgombea wa EFF ambacho ni chama cha tatu kwa ukubwa pia atatumia kaulimbiu kama hizo, kwa kuwa pia kinawapinga kwa uwazi wageni.

Vyama vingine vidogo kama Patriotic Alliance and ActionSA pia vinapinga wageni na hata vilijiongezea uungwaji mkono wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka uliopita kutokana na mtazamo huo.

Na kulingana na fikra ya Fredson Guilengue wa Wakfu wa Rosa Luxembourg wa huko Johannesburg, hali hii inatia hofu na hasa kwa kuwa uchaguzi nao unakaribia licha ya takwimu za mashambulizi zinaonyesha kupungua ikilinganishwa na mwaka 2022, akizingatia zaidi visa vinavyofanywa katika Operesheni Dudula.

Ameongeza kuwa matatizo ya Waafrika Kusini Weusi na waafrika kutoka maeneo mengine yamechangiwa na sababu kadha wa kadha, kuanzia ukoloni na ubaguzi wa rangi ambavyo vilileta mgawanyiko sio tu kati ya weupe na weusi, bali pia weusi kwa weusi.

Wahamiaji hawaleti matatizo Afrika Kusini 

Utafiti wa Taasisi ya Masomo ya Usalama, ISS ya mjini Pretoria unasema kila mtu wa pili nchini Afrika Kusini hajaajiriwa,inayoongeza umasikini, kukosekana kwa usawa wa kijamii na hata ufisadi, ingawa mara zote wageni ndio husingiziwa kufanya uhalifu.

Je, umaskini unachangia machafuko ya Afrika Kusini?

Kulingana na ISS, ukweli ni kwamba utawala mbovu na ufisadi kwenye siasa ikichanganywa na ombwe la kiutawala kwa pamoja vinachangia uhalifu na hali ya sintofahamu nchini humo.

Soma pia:Madereva wa kigeni mashakani Afrika Kusini

Taasisi hiyo imeongeza kuwa, asilimia karibu 6.5 ya wahamiaji nchini Afrika Kusini sio kubwa ikilinganishwa na maeneo mengine ulimwenguni.

Lakini pia sera mbovu ya uhamiaji imesababisha wahamiaji wengi kukosa vibali vya uhakika vya ukaazi.

ISS imesema wageni wengi wanahamia Afrika Kusinikihalali na baadaye hunyang'anywa hadhi yao ingawa hawajafanya makosa.

Wanaeleza kuwa wizara ya mambo ya ndani nayo imekumbwa na ufisadi kwa miaka mingi na ina urasimu mkubwa sana linapokuja suala la kushughulikia maombi na vibali vya ukaazi.