Serikali ya Muungano yaundwa nchini Iraq. | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.11.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Serikali ya Muungano yaundwa nchini Iraq.

Waziri mkuu, Nuri al Maliki ataendelea kulihudumia taifa katika wadhifa wake.

default

Waziri mkuu wa Iraq, Nuri al Maliki.

Sasa kuna nuru ya matumaini ya amani na maelewano nchini Iraq. Baaada ya wabunge kukutana kwa masaa mengi ya majadiliano, wamekubaliana kuunda serikali ya mseto, miezi minane baada ya uchaguzi uliozua ubishi. Hayo ni kwa mujibu wa rais wa jimbo la kabila la Wakurdi, Masoud Barzani.

Waziri mkuu Nuri al Maliki, wa madhehebu ya Washia, ataendelea kuhudumia taifa kama waziri mkuu na kambi ya Wakurdi watashikilia wadhifa wa urais.

Iyad Allawi ambaye ni mwanachama wa kambi inayoungwa mkono na Wasunni amechaguliwa kuwa mkuu wa baraza jipya litakaloshughulikia utungaji wa sera na spika wa bunge atachaguliwa kutoka katika kambi yake.

Matokeo hayo yanajiri baada ya mazungumzo ya siku tatu ya shinikizo za ndani kutoka kwa kambi za kisiasa. Hatua hiyo inatabiriwa kusitisha visa vingi vya kuvuruga usalama, vikiwemo miripuko ya kujitoa mhanga na ongezeko la uhasama wa kidini.

Marekani ilikuwa imeelezea wasiwasi wake kuhusu mazungumzo ya muda mrefu bila makubaliano kati ya wanasiasa nchi humo na ilikuwa ikishinikiza kuwepo na serikali ya mseto.

Der neue irakische Ministerpräsident Iyad Allawi

Bw Iyad Allawi amechaguliwa kuwa mkuu wa baraza jipya la utungaji sera.

Kambi ya chama cha Iraqiya cha waziri mkuu wa zamani, Iyad Allawi ambacho kilishinda uchaguzi kwa viti vichache na kilichotaka kuchukua hatamu ya uongozi kimethibitisha kwamba kimekubaliana kuunda serikali ya mseto.

Msemaji wa kambi hiyo, Intissar Allawi ambaye hakutaja mengi ya yale yaliyokubaliwa alithibitisha tu kwamba kuna mkataba.

Muungano wa wafuasi wa Kisunni uliyaunga mkono makubaliano hayo. Wafuasi hao ambao walitamalaki wakati wa utawala wa hayati Saddam Hussein, wamekuwa wakiendeleza vita dhidi ya wanajeshi wa Marekani tangu mwaka wa 2003. Wachunguzi wa kisiasa wamesema kuhusishwa kwao serikalini kutachangia pakubwa katika kusitisha mashambulio hasa yale ya kujitoa mhanga.

Wabunge watakutana saa tisa kwa saa za Afrika mashariki kumchagua Osama al-Nujaifi ambaye ni Msunni wa muungano wa Iraqiya kama spika wa bunge. Duru za bunge la Iraq zinasema kwamba kamati maalum imeundwa kushughulikia masuala mengine mazito kuhusiana na serikali hiyo ya mseto.

Matukio hayo mapya ya kisiasa yanajiri saa chache baada ya miripuko ya mabomu kutokea jana nchini humo na iliyosababisha vifo vya watu sita na ni siku chache tu baada ya Wakristo kutekwa nyara na waripuaji wa kujitoa mhanga katika kanisa la Kikatoliki waliowauwa watu 53. Ni siku moja tu pia tangu kuzinduliwa kwa kitabu cha ‘Decision Points’ cha rais wa zamani wa Marekani,George Bush ambaye alikariri kuwa Wairaqi wako huru zaidi na ulimwengu uko salama bila ya Saddam Hussein. Katika kitabu hicho, Bw Bush alisema hana nia ya kuomba msamaha kwa kuanzisha vita vya Iraq mwaka wa 2003.

Mwandishi: Peter Moss /AFP/dpa

Mhariri: Josephat Charo.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com