Serikali ya Kansela Merkel yapata pigo kubwa majimboni | Magazetini | DW | 28.03.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Serikali ya Kansela Merkel yapata pigo kubwa majimboni

Mada kuu iliyoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani, Jumatatu ya hii leo ni matokeo ya chaguzi za majimbo zilizofanywa jana katika jimbo la Baden-Württemberg na Rhineland-Pfalz.

Basi tutaanza na gazeti la HANDELSBLATT linaloeleza hivi:

Kwa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na makamu wake, Guido Westerwelle, sasa ni suala la kufa na kupona kisiasa. Kwani serikali iliyotawala vizuri kwa zaidi ya mwaka mmoja inapokuja kushindwa katika takriban chaguzi zote majimboni na wapiga kura kutowaamini tena, hata katika ngóme ya vyama vyao vya kihafidhina, CDU na kiliberali, FDP, Baden-Württemberg, basi wakati umewadia kuchunguza zile siasa zilizokuwa zikifuatwa hadi sasa. Hata viongozi wenyewe wajiulize wapi walipokwenda kombo.

Likiendelea, gazeti hilo linasema:

Viongozi waliopata pigo hilo kubwa huenda wakajaribu kutafuta sababu ambazo hazikuweza kuzuilika kutoka nje kama vile janga la nyuklia huko Japani, mzozo wa sarafu wa Euro, au operesheni ya kijeshi huko Libya. Lakini ukweli ni kwamba tangu mwanzoni serikali ya mseto ya vyama vya CDU na FDP haikuwa na msimamo dhahiri.

Nalo REUTLINGER GENERAL-ANZEIGER linasema:

Wapiga kura katika jimbo la Baden-Württemberg wameandika historia mpya kwa njia mbali mbali. Kwani kwa kuipiga teke serikali ya jimbo ya vyama vya CDU na FDP, iliyokuwa ikiongozwa na Stefan Mappus, wapiga kura hao wamekomesha enzi ya utawala wa chama cha kihafidhina cha CDU uliodumu miaka 58 mfululizo katika jimbo tajiri la Baden Württemberg. Machi 27 mwaka 2011 na matokeo yake ya kihistoria ni ushindi - kwani uchaguzi huo umedhihirisha kuwa mageuzi yanaweza kufanyika. Na hiyo kwa njia halali ya kidemokrasia.

Tunamalizia kwa gazeti la BERLINER ZEITUNG linaloeleza hivi:

Kile kilichotokea jana katika jimbo la Baden-Württemberg si mabadiliko ya kawaida ya kidemokrasia tu - bali ni mapinduzi yaliyofanywa kwa amani na utaratibu katika vibanda vya kupigia kura - na hivyo ndio inavyotakiwa. Na mapinduzi hayo hayatoleta mageuzi katika jimbo hilo la kusini magharibi tu, bali katika taifa zima la Ujerumani.

 • Tarehe 28.03.2011
 • Mwandishi Martin,Prema/DPA
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/RDQR
 • Tarehe 28.03.2011
 • Mwandishi Martin,Prema/DPA
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/RDQR