Serikali ya Guinea yazungumza na vyama vya wafanyakazi | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Serikali ya Guinea yazungumza na vyama vya wafanyakazi

Serikali ya Guinea hapo Alhamisi imekuwa na mazungumzo na vyama vya wafanyakazi vilivyohusika na vurugu zilizopelekea kutangazwa kutumika kwa sheria ya kijeshi nchini humo huku kukiwa na onyo kwamba nchi hiyo inaweza kutumbukia kwenye machafuko.

Mmojawapo ya waandamanaji aliejeruhiwa baada ya kupigwa risasi nchini Guinea

Mmojawapo ya waandamanaji aliejeruhiwa baada ya kupigwa risasi nchini Guinea

Mazungumzo hayo ya kutafuta njia za kumaliza mgomo wa taifa na kuondolewa kwa sheria ya kijeshi yanafanyika wakati wito wa kimataifa ukizidi kuongezeka kumtaka Rais Lansana Conte wa Guinea akubali suluhisho la kisiasa.

Vyama vya wafanyakazi wiki hii vilianza tena maandamano mapya dhidi ya utawala wa Rais Lansana Conte alie mkongwe ambapo wakati wa siku mbili za mgomo wa taifa rais huyo ameamuru kutumika kwa sheria ya kijeshi nchini kote.

Mtu mmoja zaidi ameuwawa hapo Alhamisi katika mji ulioko mikoani na kufanya idadi ya watu waliouwawa na wanajeshi kwa kukaidi masharti makali ya sheria hiyo ya kijeshi kufikia tisa ambapo kwayo wanajeshi wamepewa amri ya kufyatuwa risasi wakati wanapokabiliwa na upinzani au tishio la kushambuliwa.

Spika wa bunge Aboubakar Sompare ambaye kwa mujibu wa katiba atachukuwa nafasi ya urais iwapo mkuu wa nchi atavuliwa madaraka ameitisha mazungumzo hayo yanayohudhuriwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi,wawakilishi wa kijeshi kadhalika viongozi wa kidini na wale wa kibiashara.

Habari kamili juu ya mazungumzo hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika tokea Conte atangaze sheria ya kijeshi kupambana na maandamano ya upinzani yaliogharimu maisha ya watu 113 hazikuweza kupatikana mara moja.

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Alpha Oumar Konare amemuandikia Rais Conte aliyetawala Guinea tokea mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1984 yasiokuwa na umwagaji damu kupinga hatua yake ya kulitumia jeshi kama zana dhidi ya raia.

Katika baruwa yake hiyo kwa Conte ambaye ni mgonjwa wa kisukari na mwenye kupoteza kumbukumbu na ambaye pia amegundulika kuwa na kansa ya damu Konare amelaani matumizi ya nguvu kubwa kipindukia za kijeshi dhidi ya raia kulikosababisha kupotea kwa maisha ya watu wengi.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais John Kufour wa Ghana akizungumza katika mkutano wa Viongozi wa Ufaransa na Afrika mjini Cannes Ufaransa pia ametaja umuhimu wa kuupatia ufumbuzi mzozo huo wa Guinea unaohusisha mauaji ya raia.

Kufour ametowa wito kwa rais na kwa serikali ya Guinea kutumia njia zote za amani kuirudisha nchi hiyo kwenye hali ya kawaida na kwamba Umoja wa Afrika uko tayari kutowa ushirikiano na msaada wake kufikia ufumbuzi wa haraka wa mzozo huo.

Bunge la Umoja wa Ulaya limetowa wito wa kuundwa kwa tume ya uchunguzi ya kimataifa chini ya himaya ya Umoja wa Mataifa kuwatambuwa na kuwafikisha mbele ya sheria wale waliohusika na mauaji na uvunjaji wa haki za binaadamu nchini humo.Ujerumani ambayo inashikilia Urais wa Umoja wa Ulaya imesema ina wasi wasi kutokana na vurugu hizo na kuiita kuwekewa vikwazo kwa uhuru ni hatua ya kurudi nyuma Jopo la kimataifa limeonya kwamba hali nchini Guinea inaweza kugeuka haraka kuwa ya umwagaji damu mkubwa.

Guinea iko katika amri kali ya kutotembea nje ambapo watu wanaruhusiwa kubakia nje kwa masaa sita tu kwa siku hadi hapo Februari 23 na jeshi lina madaraka ya kuchukuwa hatua zozote zile zinazohitajika kudumisha utulivu.

 • Tarehe 16.02.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHK1
 • Tarehe 16.02.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHK1

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com