1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Santorum ashinda majimbo ya Alabama na Mississippi

14 Machi 2012

Rick Santorum amepata ushindi kwenye majimbo mawili ya kusini katika uchaguzi unaoendelea nchini Marekani, kumteua mtu atakayegombea kwa niaba ya chama cha Republican dhidi ya Rais Barack Obama mwezi Novemba.

https://p.dw.com/p/14KGa
Rick Santorum anaonekana kushinda nyoyo za wahafidhina wa chama cha Republican
Rick Santorum anaonekana kushinda nyoyo za wahafidhina wa chama cha RepublicanPicha: dapd

Ushindi wa asilimia 35 katika jimbo la Alabama, na asilimia 33 katika jimbo jirani la Mississippi, umeyapa uzito madai ya Rick Santorum kuwa yeye ndiye anayebeba bendera ya wahafidhina ndani ya chama cha Republican, dhidi ya Mitt Romney ambaye anaongoza katika uchaguzi wa majimbo wa chama hicho, kumtafuta mwakilishi wake atakayepambana na Rais Barack Obama katika uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba mwaka huu.

Katika majimbo hayo ya kusini ambayo ni ngome ya wahafidhina wa chama cha Republican, spika wa zamani wa baraza la wawakilishi, Newt Gingrich amekuja katika nafasi ya pili. Kwake hilo ni pigo kubwa, kwani alihitaji kupata ushindi katika majimbo hayo ili kuiokoa ndoto ya kampeni yake ambayo inazidi kudidimia.

Newt Gingrich anakabiliwa na shinikizo la kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hiki.
Newt Gingrich anakabiliwa na shinikizo la kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hiki.Picha: AP

Romney ashindwa kuwapiga kumbo wapinzani

Lakini pia ni kikwazo kwa Mitt Romney, ambaye amashindwa kuwapiga kumbo wapinzani wake, na kuwashawishi wapiga kura kuwa yeye ndiye mgombea mwenye nguvu kukabiliana na Rais Barack Obama katika uchaguzi ambao unabakiza miezi tu kufanyika.

Rick Santorum ametumia ushindi huu kuwatolea wito wahafidhina kuungana nyuma yake.

''Wakati umewadia kwa wahafidhina kujiweka pamoja.Wakati umewadia, kuhakikisha kwamba tunakuwa katika nafasi nzuri kushinda uchaguzi huu, na kuwa katika nafasi nzuri ni kumteua mhafidhina kusimama dhidi ya Barack Obama na kukabiliana naye kwa hoja zote.'' Alisema Santorum.

Santorum amemkejeli Mitt Romney kushindwa kupata ushindi katika majimbo kadhaa licha ya kutumia pesa zaidi ya wapinzani wengine wote kujitangaza.

Licha ya kushinda majimbo mengi zaidi, Mitt Romney ameshindwa kuwapiga kumbo wapinzani wake
Licha ya kushinda majimbo mengi zaidi, Mitt Romney ameshindwa kuwapiga kumbo wapinzani wakePicha: AP

Wito kwa wahafidhina kujiweka pamoja

Macho yote sasa yanamuangalia Newt Gingrich ambaye ameshinda majimbo mawili tu kati ya 26 yaliyokwishafanya uchaguzi. Anakabiliwa na miito inayozidi kuongezeka kumtaka ajiondoe kwenye kinyang'anyiro hiki, ili kukusanya kura za wahafidhina nyuma ya Rick Santorum.

Licha ya shinikizo hilo lakini, Gingrich amesema ataendeleza mapambano hadi mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika mwezi Agosti mjini Tampa katika jimbo la Florida, kumteua mgombea rasmi wa chama cha Republican.

Mbio za watu wawili

Kambi ya Rick Santorum inachukulia kushindwa kwa Newt Gingrich katika majimbo ambayo ni ya karibu na nyumbani kwake, kama sababu ya kumlazimisha kujiengua kwenye uchaguzi huu. Msemaji wa Santorum Allison Stewart amekiambia kituo cha Televisheni cha CNN, kuwa kuanzia sasa, mapambano yatakuwa baina ya watu wawili, ambao ni Rick Santorum, na Mitt Romney.

Msemaji huyo amedai kuwa Rick Santorum ndiye mgombea anayewakilisha maoni tofauti na ya Rais Barack Obama, na kwamba wananchi wameanza kuyang'amua hayo.

Romney ambaye amekuja katika nafasi ya tatu katika majimbo ya Alabama na Mississippi, anaongoza kwa kujikusanyia kura nyingi za uteuzi, akiwa tayari na asilimia 40 ya kura 1,144 anazohitaji mtu kuweza kuteuliwa kuwa mgombea rasmi wa chama.

Upande wa Santorum unasema itakuwa kazi ngumu kwa Romney kufikisha wingi wa kura za uteuzi anazohitaji kupitishwa kuwa mgombea wa chama cha Republican, na katika kitabu chao cha kampeni wameandika kuwa ''huu ni wakati wao''.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri:Hamidou Oummilkheir