1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Romney aongoza chaguzi za awali

7 Machi 2012

Mitt Romney ambaye ni mgombea mwenye matumaini ya kuwania kiti cha urais nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, katika chaguzi za awali zilizofanyika jana, alijipatia ushindi muhimu katika majimbo sita.

https://p.dw.com/p/14GGV
Mitt Romney akiwa na watu wanaomuunga mkono
Mitt Romney akiwa na watu wanaomuunga mkonoPicha: AP

Jana ilikuwa siku ya muhimu kisiasa kwa Marekani kwani chaguzi za awali za kumtafuta mgombea wa urais wa chama cha Republican zilifanyika katika majimbo kumi. Kutokana na umuhimu wake, siku hiyo inapewa jina la Super Tuesday. Gavana wa zamani wa jimbo la Massachusetts, Mitt Romney, aliweza kujipatia ushindi katika jimbo lake la Massachusetts na pia katika majimbo ya Virginia, Idaho, Wyoming na Alaska na pia katika jimbo la Ohio ambalo linapewa umuhimu zaidi.

Katika uchaguzi uliofanyika jana, Mitt Romney alipata asilimia 38 ya kura zilizopigwa katika jimbo la Ohio na hivyo kumshinda mpinzani wake wa karibu Rick Santorum aliyepata asilimia 37 ya kura. Ushindi katika jimbo la Ohio unapewa umuhimu mkubwa kwani wachambuzi wanaamini kwamba anayeshinda uchaguzi katika jimbo hilo ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuwa mshindi wa jumla wa chaguzi za awali na hivyo kuwa mgombea wa urais wa chama cha Republican.

Rick Santorum aendelea kuwa mpinzani wa karibu wa Romney
Rick Santorum aendelea kuwa mpinzani wa karibu wa RomneyPicha: AP

Santorum bado ni mpinzani wa karibu

Rick Santourm pia alifanikiwa kupata ushindi katika baadhi ya majimbo. Miongoni mwao ni majimbo ya Tennessee na Oklahoma ambayo wakaazi wake ni wahafidhina. Matokeo hayo yanampa moyo Santorum kwamba ataweza kushinda chaguzi zijazo katika majimbo mengine kama vile Kentucky na West Virginia. Wachambuzi wanasema kwamba Mitt Romney hakubaliki sana katika majimbo hayo. Watu wengi wanamwona kama tajiri mkubwa wa tabaka la juu anayetoka katika eneo la Marekani Mashariki linalochukiwa na wengi. Wengi hawaamini kwamba Romney ataweza kuiliongoza taifa la Marekani kuwa taifa lenye nguvu na linalofuata maadili ya kikristo.

Rick Santorum anakubalika zaidi. Usiku wa jana alikazia msingi wa kile anachokiamini: "Marekani imekuwa taifa kubwa," alisema Santorum. "Tumeweza kujenga taifa jipya. Sasa tunahitaji watu watakaompinga rais Obama na maono yake juu ya udhibiti wa serikali katika sekta ya afya, nishati, huduma za kifedha na mambo mengine."

Newt Gingrich apata ushindi nyumbani

Newt Gingrich aliyekuwa mwenyekiti wa kambi ya wanachama wa Republican katika bunge la Marekani jana alijipatia ushindi katika jimbo lake la Georgia. Mke wake, Callista Gingrich, alisema kwamba ushindi huo unamtosha mumewe kubakia katika kinyang'anyiro cha kiti cha urais. Alipokuwa akizungumza na wapiga kura, alimtambulisha mumewe kama rais mtarajiwa wa Marekani.

Newt Gingrich akiwa na mke wake Callista
Newt Gingrich akiwa na mke wake CallistaPicha: dapd

Jambo hilo linaonekana kama kichekesho kwani Gingrich amepata kura chache sana katika uchaguzi wa jana na hivyo hana nafasi ya kuwa mgombea wa urais wa chama cha Republican, au hata kuwa rais. Ron Paul mwenye umri wa miaka 72 pia hatarajiwi kuwa mshindi wa jumla wa chaguzi za awali. Mwanasiasa huyo kutoka jimbo la Texas mara kwa mara anaonekana kama mtu anayetoa matamko yanayofurahisha lakini jana hakushinda uchaguzi hata katika jimbo moja. Wapo wanachama wenzake wengi wanaomshauri ajiondoe katika kinyang'anyiro hiki.

Mwandishi: Silke Hasselmann/Elizabeth Shoo

Mhariri: Josephat Charo