1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya kwanza ya rais Medvedev katika nchi ya Ulaya magharibi.

Mtullya, Abdu Said5 Juni 2008

Rais D.Medvedev wa Urusi aanza ziara nchini Ujerumani ambayo ni ya kwanza katika nchiya magharibi tokea aapishwe kuwa rais wa nchi yake.

https://p.dw.com/p/EE4R
Rais Medvedev na mwenyeji wake Kansela Angela Merkel mjini Berlin.Picha: picture-alliance/ dpa

Rais Dimitry Medvedev wa Urusi leo anaanza ziara nchini Ujerumani ambayo ni ya kwanza katika nchi ya magharibi tokea aapishwe mwezi mmoja uliopita, kuiongoza Urusi.

Katika ziara hiyo rais Medvedev anatarajiwa kufanya mazungumzo na Kansela Merkel ,rais Horst Köhler na waziri wa mambo ya nje Frank- Walter Steinmeier.

Masuala yanayotazamiwa kuzingatiwa kwenye mazugumzo hayo ni pamoja na mikutano inayotarajiwa kuanza, kujadili mkataba wa ushirikiano wa muda mrefu baina ya Urusi na Umoja wa Ulaya, masuala ya nishati na juu ya matayarisho ya mkutano wa nchi nane tajiri duniani G8 utakaofanyika Japan. Suala la haki za binadamu pia linatarajiwa kupewa uzito katika mazungumzo hayo baina ya rais Medvedev na wenyeji wake wa Ujerumani.

Rais Medvedev wa Urusi anafanya ziara hiyo wakati ambapo uhusiano baina yake na Ujerumani umeendelea kuwa mahsusi.

Ujerumani na Urusi zina uhusiano mzuri katika sekta za uchumi, biashara na nishati. Wizara ya uchumi ya Urusi imesema biashara baina ya nchi mbili hizo inatarajiwa kustawi kwa asilimia 25 yaani, thamani ya Euro bilioni 40 mnamo mwaka huu.

Katika ziara yake nchini Ujerumani rais Medvedev atajadili njia za kuiwezesha Urusi kuekeza vitega uchumi zaidi katika nchi za Ulaya magharibi.Hatahivyo katika mazungumzo na wenyeji wake rais Medvedev hatakwepa suala la haki za binadamu.