Rais Recep Tayyip Erdogan amuonya jenerali Haftar dhidi ya mashambulizi zaidi | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.01.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais Recep Tayyip Erdogan amuonya jenerali Haftar dhidi ya mashambulizi zaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema mbabe wa kivita wa Libya, Jenerali Khalifa Haftar, ameondoka nchini Urusi bila ya kutia saini mkataba wa kusitisha mapigano .

Akihutubia mjini Ankara muda mfupi uliopita, Rais Erdogan amesema kuwa hawatasita kumpa fundisho kamanda huyo wa wapiganaji wa mashariki mwa Libya, ikiwa vikosi vyake vitaendelea kuishambulia serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli.Kauli hii kali ya Erdogan inafuatia hatua ya Jenerali Haftar kuondoka mjini Moscow, Urusi, bila kuweka saini makubaliano ya kusitisha mapigano yanayoendelea kwa miezi sita sasa kuwania udhibiti wa mji mkuu, Tripoli.

Urusi na Uturuki zilikuwa zinajaribu upatikane mkataba wa kudumu wa kusitisha mapigano wakati wa mazungumzo katika mji mkuu wa Urusi hapo jana, Jumatatu, ambayo yaliyotarajiwa kuwaleta pamoja Jenerali Haftar na mkuu wa serikali yenye makao yake mjini Tripoli, Fayez al-Seraj. Al-Seraj alitia saini mktaba huo lakini Haftar anayeongoza jeshi la waasi lenye makao yake katika eneo la mashariki mwa Libya, alitaka muda hadi leo Jumanne kufikiria suala hilo, lakini baadaye imefahamika kuwa ameondoka hivi leo mjini Moscow bila hata kutia saini makubaliano hayo.

Hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema:

"Mafanikio madogo yamepatikana. Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa, Al-Serraj, na rais wa baraza kuu la kitaifa la Libya, al-Mishri, wametia saini mkataba huo. Kamanda wa jeshi la kitaifa la Libya, Khalifa Haftar, na spika wa bunge la Libya mjini Tobruk, Aguila Saleh, waliidhinisha mkataba huo na kuomba muda zaidi kuuzingatia hadi kesho asubuhi kuamua kutia saini. Natumai uamuzi huo utakuwa wa makubaliano."

LNA Chef Khalifa Haftar

Kamanda wa kikosi cha jeshi la LNA

Shirika la habari la Urusi, TASS limemnukuu waziri huyo wa mambo ya kigeni akisema kuwa Haftar ameondoka nchini humo mapema leo. Kulingana na kituo cha televisheni cha Al Arabiya Haftar akisema kuwa rasimu ya mkataba imepuuza matakwa mengi ya jeshi lake, analoliita jeshi la kitaifa la Libya. Mwakilishi wa serikali inayohusishwa na Haftar alikuwa ametia saini mkataba huo na kutoa matumaini ya muda kwamba kamanda huyo hatimaye angetia saini mkataba huo.

Haftar alikataa kutia saini mkataba huo wa kusitisha mapigano kwa sababu haukujumuisha muda wa mwisho wa kuvunjilia mbali vikosi vya serikali. Hii ni kulingana na shirika la habari la Interfax lililonukuu duru za jeshi lake.Kushindwa kwa Haftar kutia saini mkataba huo katika mazungumzo yaliyoongozwa na Uturuki na Urusi, huenda kukakatiza juhudi za kidiplomasia za kuidhibiti hali ilivyo nchini Libya ambayo imekumbwa na ghasia tangu kupinduliwa kwa serikali ya Muammar Gaddafi mnamo mwaka 2011.

Siku ya Jumamosi, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema kuwa anapanga kuandaa mkutano kuhusu Libya siku ya Jumapili pamoja na viongozi kutoka Uturuki, Urusi na Italia. Licha ya Lavrov kuthibitisha kuwa mazungumzo hayo yalimalizika bila ya ufanisi akiwa katika ziara nchini Sri Lanka, alisema kuwa Urusi na Uturuki zitazidi kushinikiza kupatikana suluhisho kwa njia ya mazungumzo.

Mazungumzo ya jana Jumatatu yalitarajiwa kuweka rasmi mkataba wa muda wa kusitisha mashambulizi ulioafikiwa siku ya Jumapili lakini mkataba huo haukutekelezwa kikamilifu na kuna ripoti ya mapigano kuendelea nchini Libya.

Taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta lina serikali mbili pinzani. Serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inayoongozwa na al-Serraj mjini Tripoli na nyingine yenye makao yake katika mji wa Tobruk, Mashariki mwa Libya inayoongozwa na Haftar.