Rais Putin aonywa juu ya njama ya kumuuwa akiwa ziarani Iran. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 15.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Rais Putin aonywa juu ya njama ya kumuuwa akiwa ziarani Iran.

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameonywa na majasusi wake maalum juu ya uwezekano wa kuwepo kwa njama ya kumuuwa wakati wa ziara yake nchini Iran wiki hii.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Iran imetupilia mbali kuwa haina msingi repoti iliotolewa na shirika la habari la Urusi mInterfax kwamba washambuliaji wa kujitolea muhanga maisha wamejiandaa kumshambulia rais huyo. Imeyaelezea madai hayo kuwa ni vita vya kisaikolojia vilivyopangwa na maadui wa serikali ya Iran ikimaanisha mataifa ya magharibi kwa dhamira ya kudhoofisha uhusiano kati ya Urusi na Iran.

Naibu msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba alikuwa hajuwi juu ya kuwepo kwa mipango yoyote ile ya kufuta ziara hiyo ya Putin. Hii ni ziara ya kwanza kufanywa na mkuu wa Urusi nchini Iran tokea Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na inakuja wakatui kukiwepo mvutano juu ya mpango wa nuklea wa Iran.

Alipotakiwa azungumzie juu ya repoti ya vyombo vya habari vya Urusi juu ya njama hiyo ya kumuuwa Putin Peskov amesema kwa njia ya simu kutoka Tehran kuwa habari hizo zinashughulikiwa na makachero na kwamba rais amejulishwa.

Shirika la habari la Interfax limeripoti hapo jana kwamba mashushu wameelezwa kwamba washambuliaji wa kujitolea muhanga na wateka nyara wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya kumuuwa au kumteka nyara Putin wakati wa ziara yake nchini Iran ambayo imepangwa kuanza hapo kesho.

Kwa mujibu wa shirika hilo duru za kuaminika kutoka kwa mojawapo wa majasusi wa Urusi zimepata habari kutoka duru kadhaa nje ya Urusi kwamba wakati wa ziara ya Putin nchini Iran njama ya kumuuwa imekuwa ikiandaliwa.

Shirika hilo ambalo ni mojawapo ya mashirika yenye maingiliano maalum na Ikulu ya Urusi halikutowa ufafanuzi zaidi duru hizo ni akina nani au iwapo zinahusiana na serikali za mataifa ya magharibi.

Rais Putin amewasili katika mji wa Wiesbaden nchini Ujerumani hapo jana usiku kwa mazungumzo na Kansela Angela Merkel ambayo yanatarajiwa pia kuijadili Iran.Alipoulizwa mwenyewe juu ya repoti ya njama hiyo alipunga mkono wa mapuuza na kusema potom akimaanisha baadae.

Shirika la habari la kiserikali nchini Iran likikariri duru za kuaminika limesema ziara hiyo itaendelea kufanyika.

Limesema wanasiasa wa mataifa ya magharibi na vyombo vyao vya habari wamekuwa wakijaribu kumshawishi Putin achukuwe hatua ya kisiasa kwa kutosafiri kwenda Iran na kwamba kwa vile sasa wameshindwa kwa hilo wanakusudia kumshawishi asisafiri kwenda Iran kutokana na masuala ya usalama na uvumi wa njama ya kumuuwa.

Putin ambaye atakuwa mkuu wa kwanza wa Kremlin Ikulu ya Urusi kuitembelea Iran tokea Dikteta wa muungano wa Urusi Joseph Stanlin kuitembelea nchi hiyo hapo mwaka 1943 atakuwepo rasmi nchini Iran kwa mkutano wa viongozi wa mataifa ya Bahari ya Caspian.

Lakini mkutano wake na Rais Mahamoud Ahmedinejad wa Iran unaweza kumpa nafasi ya kutafuta muafaka wa amani juu ya mpango wa nuklea wa Iran na kuonyesha kwamba ni mtu mwenye mawazo huru mbali na Marekani katika masuala ya Mashariki ya Kati.

Urusi inasema kuzungumza na Iran ni njia yenye tija katika kushughulikia mpango wake wa nuklea kuliko kuitenga nchi hiyo.

Inaiuzia nchi hiyo silaha kwa kukaidi mashaka ya Marekani na inajenga kituo cha kuzalisha umeme kwa nguvu za nuklea kwa ajili ya Iran huko Bushehr katika Ghuba ya Uajemi.

 • Tarehe 15.10.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C77n
 • Tarehe 15.10.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C77n

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com