Rais Obama akutana na Waziri Mkuu Putin | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.07.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais Obama akutana na Waziri Mkuu Putin

Rais wa Marekani Barack Obama kwa mara ya kwanza amekutana uso kwa uso na Waziri Mkuu wa Russia Vladimir Putin leo hii mjini Moscow kwa mazungumzo yaliyopindukia muda uliopangwa kwa zaidi ya dakika thelathini

US President Barack Obama talks with Russian Prime Minister Vladimir Putin during a meeting at Putin's home Novo Ogaryovo in Moscow, Russia 07 July 2009. President Obama is in Moscow to meet with Russian President Dmitryi Medvedev and Prime Minister Vladimir Putin prior to the G8 Summit in Italy later this week. EPA/SHAWN THEW +++(c) dpa - Report+++

Rais wa Marekani Barack Obama(kulia) akizungumza na Waziri Mkuu wa Russia Vladimir Putin mjini Moscow Julai 07,2009.

Rais Obama na Waziri Mkuu Putin wakati wa mazungumzo yao yaliyoelezwa kuwa wazi, walibadilishana maoni yao kuhusu maslahi ya Russia na Marekani. Vile vile walijadili masuala yanayohusika na Iran,mabadiliko ya hali ya hewa,mtikisiko wa uchumi, utapakaji wa silaha za nyuklia na ugaidi.Mazungumzo hayo yalikuwa wazi na viongozi hao wameeleza matumaini ya kuweza kuuweka uhusiano wa nchi hizo mbili katika msingi mpya. Waziri Mkuu Putin alisema:

"Uhusiano kati ya Russia na Marekani umepitia awamu mbali mbali. Kulikuwepo kipindi kizuri na wakati mgumu. Uhusiano huo vile vile umeshuhudia marumbano. Sasa, jina lako Obama, tunalifungamanisha na matumaini ya kuendeleza uhusiano wetu."

Kwa upande wake,Obama alisema kuwa Russia na Marekani zinapaswa kuendeleza uwazi na utawala wa kisheria ili kuhakikisha ukuaji wa kiuchumi na uwekezaji.Amesema kuwa angependa kuona biashara kati ya nchi hizo mbili ikipindukia kiwango cha hivi sasa cha dola bilioni 36 kwa mwaka.

Na kuhusu Georgia, jamhuri ya zamani ya iliyokuwa Soviet Union, ambayo mwaka jana ilipigana vita vifupi na Russia,Obama alikariri kuwa hakubaliani na msimamo wa Russia kuhusu mgogoro huo. Hapo awali, Obama alipotoa hotuba yake katika chuo cha biashara mjini Moscow, alisema:

"Historia inatuonyesha kuwa serikali zinazotumikia umma wake, hudumu na huimarika, kinyume na zile zinazoshughulikia maslahi ya mamlaka yake yenyewe. Na serikali zinazowakilisha matakwa ya wananchi wake, hazipo hatarini kushindwa kuongoza, kuwatesa wananchi wake au kuanzisha vita dhidi ya wengine."

Obama vile vile, ametoa wito kwa Russia kushiriki katika jitahada za kuzuia utapakaji wa silaha za nyuklia hasa nchini Iran na Korea ya Kaskazini. Amesema Russia na Marekani kama madola makuu yenye nguvu za kinyuklia, zina jukumu maalum. Hakuna atakaenufuaika katika mashindano ya kujipatia silaha za nyuklia huko Asia ya Mashariki au katika Mashariki ya Kati.

Na katika hatua inayotazamwa kama jitahada ya kuituliza Russia,Rais Obama amesema hakutokuwepo haja ya kuweka mfumo wa ulinzi katika nchi za Ulaya ya Mashariki ikiwa kitisho cha mradi wa nyuklia wa Iran na makombora yake, kitaondoshwa. Russia inapinga vikali mpango wa Marekani kutaka kuweka makombora ya kinga katika nchi za Ulaya ya Mashariki.Marekani inashikilia kuwa huo ni mfumo wa kujikinga dhidi ya kile kilichoitwa mataifa korofi.

Mwanzoni mwa ziara yake hiyo ya siku mbili mjini Moscow Rais Obama alikutana na Rais wa Russia Dmitry Medvedev. Viongozi hao walifungua ukurasa mpya katika uhusiano wa nchi hizo mbili. Kimsingi walikubaliana kuwa kuna haja ya kuwa na mkataba mpya kuchukua nafasi ya mkataba wa sasa wa kupunguza silaha za nyuklia uitwao START na unaomalizika mwisho wa mwaka huu. Viongozi hao vile vile wamesema kuwa Russia imekubali kuiruhusu Marekani kutumia anga yake kusafirisha mahitaji ya kijeshi yanayohusika na operesheni za nchini Afghanistan. Lakini hatua muhimu iliyotangazwa na Obama na Medvedev inahusika na makubaliano ya kupunguza idadi ya vichwa vya makombora vinavyodhibitiwa na nchi hizo mbili.

Rais Obama kesho Jumatano, anatazamiwa nchini Italia ambako atahudhuria mkutano wa kilele wa nchi nane tajiri zilizoendelea kiviwanda duniani G-8.

Mwandishi: P.Martin / DPAE

Mhariri: S.Kitojo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com