Rais mpya wa Ujerumani achaguliwa leo
30 Juni 2010Baraza hilo maalum hujumuisha wabunge wa serikali kuu ya Berlin,wa serikali za majimbo 16 na wajumbe wa kiraia kutoka tabaka mbali mbali za jamii.Kawaida baraza hilo hukutana kila baada ya miaka mitano kumchagua rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Lakini, baada ya Horst Köhler kuwa rais wa kwanza kujiuzulu kabla ya kumaliza muhula wake,baraza hilo halina budi kumchagua mrithi wake. Kwani kuambatana na kipengele cha 54 cha Katiba ya Ujerumani, baraza hilo linapaswa kukutana ili kumchagua rais mpya katika kipindi cha siku thelathini kufuatia kujiuzulu kwa rais. Na leo ni siku 30 tangu Horst Köhler alipojiuzulu.
Wajumbe wa kiraia katika baraza hilo maalum, hutokea tabaka mbali mbali za kiraia kama vile fasihi,sanaa au spoti yaani ni watu mashuhuri katika jamii. Wanaweza pia kuwa wanasiasa lakini hilo si lazima. Na baraza hilo linalokutana hivi punde, lina wajumbe 1244. Katika kura zitakazopigwa hii leo kumchagua rasi mpya, serikali kuu ya muungano wa vyama ndugu vya CDU/CSU na chama cha kiliberali FDP inatazamiwa kuwa na uwingi wa kati ya kura 645 hadi 647 kuliko ule uwingi unaohitajiwa kushinda.
Vyama hivyo tawala vimemteua mwanachama wa CDU-Waziri Mkuu wa Jimbo la Niedersachsen, Christian Wulff mwenye umri wa miaka 51, kushika wadhifa wa urais. Kwa upande mwingine, vyama vya upinzani vya SPD na Kijani vinamuunga mkono mwanaharakati wa haki za binadamu wa Ujerumani ya Mashariki ya zamani Joachim Gauck alie maarufu miongoni mwa raia.Yeye ni mgombea huru asie na chama. Ikiwa padri huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 70 atamshinda Wulff, hilo litakuwa pigo kubwa kwa serikali ya Kansela Angela Merkel na hata kusababisha mzozo wa kisiasa.
Umaarufu wa Kansela Merkel umepungua tangu alipochaguliwa tena Septemba iliyopita. Sababu kuu ni migogoro ndani ya serikali yake ya muungano pamoja na vile alivyoukabili mzozo wa kanda inayotumia sarafu ya Euro. Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni na gazeti maarufu la Kijerumani "Bild" umeonyesha kuwa asilimia 48 ya Wajerumani wanamtaka Merkel ajiuzulu ikiwa Wulff alieteuliwa na serikali ya muungano hatochaguliwa rais hii leo. Wanaosema abakie madarakani ni asilimia 30. Nchini Ujerumani,wadhifa wa rais kwa sehemu kubwa ni cheo cha heshima na Horst Köhler alikuwa maarufu miongoni mwa raia - na Wajerumani wanatoa umuhimu nani anaewaakilisha kimataifa.
Mwandishi:D.Scheschkewitz/ZPR/P.Martin/DPA/AFPE
Mhariri,Charo,Josephat