Rais Abbas aomba msaada wa Marekani
25 Septemba 2005Gaza:
Rais Mahmoud Abbas wa Palestina leo ameiomba serikali ya Marekani ishinikize Israeli iache kushambulia Ukanda wa Gaza. Amesema kuwa sasa wamerudi walikotoka na utulivu unahitajiwa tena. Wapalestina na Waisraeli wanahitaji maisha ya amani na ya kawaida. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan amesema mjini New York kuwa ana wasiwasi mkubwa na kile kinachotokea kwani uwezekano wa kuafikiana baada ya Waisraeli kuondoka katika Ukanda wa Gaza huenda ukasambaratishwa. Amewaomba Wapalestina kutekeleza kikamilifu mwito wa Rais wao, Mahmoud Abbas wa kujenga jamii ya kidemokrasia. Wanajeshi wa angani wa Israeli wameyashambulia malengo ya Wapalestina jana na usiku wa kuamkia leo baada ya Wapalestina wenye itikadi kali kushambulia mji wa mpakani wa Zderot. Mashahidi wamesema kuwa Wapalestina kadhaa wameuawa na kujeruhiwa.