1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Hungary wajitokeza kwa wingi katika uchaguzi

12 Aprili 2026

Raia wa Hungary wamepiga kura katika uchaguzi muhimu unaoweza kumaliza utawala wa miaka 16 wa Waziri Mkuu Viktor Orban na kutikisa siasa za Ulaya na Marekani.

https://p.dw.com/p/5C3b5
Hungary Budapest 2026 | Uchaguzi
Wapiga kura wa Hungary wakiwa kwenye foleni wakisubiri kupiga kura.Picha: Denes Erdos/AP Photo/picture alliance

Ushiriki wa wapiga kura umekuwa mkubwa, foleni ndefu zikiripotiwa mjini Budapest. Wapiga kura walionekana kugawanyika kati ya wanaotaka mabadiliko kutokana na gharama kubwa za maisha na madai ya ufisadi, na wale wanaotaka Orban aendelee kusalia madarakani kwa sababu ya sera zake za ustawi.

Uchaguzi huu unafuatiliwa kwa karibu na Umoja Ulaya, kwani matokeo yanaweza kuathiri uhusiano wa Hungary na Urusi, pamoja na ufadhili muhimu wa Umoja huo kwa Ukraine.

Kura zilianza kupigwa mapema asubuhi huku Orbán na mpinzani wake mkuu Péter Magyar wakipiga kura zao mjini Budapest. Orbán amesema ana imani ya kushinda, wakati Magyar akieleza uchaguzi huo kama chaguo kati ya mwelekeo wa Mashariki au Magharibi, pamoja na uwazi au propaganda.

Katika miaka yake madarakani, Orbán amekosolewa kwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na haki za makundi ya walio wachache, pamoja na kudhoofisha taasisi za serikali, madai ambayo anayakanusha.

Hata hivyo, Magyar ameibuka kuwa mpinzani mkubwa, akiahidi kushughulikia ufisadi, kuboresha huduma za afya na usafiri, na kurejesha Hungary katika mkondo wa demokrasia za Ulaya.

Matokeo ya uchaguzi huu yanaweza kuamua mustakabali wa kisiasa wa Hungary na nafasi yake ndani ya Ulaya.