JD Vance awasili Hungary kuimarisha kampeni ya Orbán
7 Aprili 2026
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amewasili nchini Hungary katika ziara inayotazamwa kwa makini na jumuiya ya kimataifa. Ziara hii inajiri siku chache tu kabla ya uchaguzi muhimu ambao wachambuzi wengi wanasema unaweza kumwangusha Waziri Mkuu wa muda mrefu, Viktor Orban.
Orban, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2010 na anajulikana kwa msimamo wake mkali wa utaifa na ukosoaji wa Umoja wa Ulaya, anakabiliwa na ushindani mkubwa kabisa katika maisha yake ya kisiasa. Tafiti huru zinaonyesha kuwa chama chake cha Fidesz kinaweza kushindwa na mpinzani wake wa mrengo wa wastani, Peter Magyar, wa chama cha Tisza.
Makamu wa Rais JD Vance, ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais Donald Trump, amemsifia Orban hadharani, akisema uhusiano kati ya Marekani na Hungary ni muhimu sana. Akiwa na mke wake Usha, Vance amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary, Peter Szijjarto, ambaye amesema ziara hiyo ni sawa na "enzi mpya ya dhahabu” katika uhusiano wa mataifa hayo mawili.
Viongozi hao wanatarajiwa kujadili masuala ya uhamiaji, usalama wa kimataifa, na ushirikiano wa kiuchumi na nishati. Vyombo vya habari vimeripoti kuwa kampuni ya mafuta ya Hungary, MOL, inapanga kununua tani laki tano za mafuta kutoka Marekani kwa takribani dola milioni 500.
Hatma ya Hungary iko mikoni mwa raia
Lakini si kila mtu anayefurahia ziara hii. Mpinzani wa Orban, Peter Magyar, ameonya dhidi ya kile anachokiita "uingiliaji wa kigeni,” akisisitiza kuwa historia ya Hungary "haiandikwi Washington, Moscow, au Brussels, bali kwenye mitaa na viwanja vya Hungary.”
Orban amekuwa akikosolewa kwa kile anachokiita "demokrasia isiyo ya kiliberali,” inayofanana na baadhi ya misimamo ya kisiasa ya Marekani katika miaka ya karibuni—hasa kuhusu uhamiaji, vyombo vya habari, na taasisi za kimataifa. Pia amekuwa na msimamo tofauti na Umoja wa Ulaya kuhusu vita vya Ukraine.
Katika mkutano na waandishi wa habari, JD Vance ameishutumu jumuiya ya Umoja Ulaya kwa "kuingilia uchaguzi wa Hungary,” akidai kuwa wamejaribu kudhoofisha uchumi wa Hungary na kupandisha gharama za maisha.
"Nataka kutoa ujumbe kwa kila mtu, hasa kwa watendaji wa serikali, maafisa na wataalamu wanaosimamia shughuli za utawala wa umma na kutekeleza sheria, sera, na kanuni huko Brussels. Watendaji hao wamefanya kila wawezalo kuwabana wananchi wa Hungary kwa sababu hawampendi kiongozi ambaye amesimama kwa ajili ya kuwatetea watu wa Hungary.”
Hata hivyo wachambuzi wanasema pamoja na msaada wa Marekani, hatima ya uchaguzi wa Hungary huenda ikaamuliwa zaidi na masuala ya ndani kama vile gharama ya maisha na uchumi.
Ziara ya Vance pia inafanyika wakati Marekani inakabiliwa na changamoto zake ikiwemo vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati na kupanda kwa bei ya mafuta, mambo yanayompa Rais Trump wakati mgumu kisiasa.
Kwa sasa macho yote yameelekezwa Budapest, ambako kura ya Jumapili inaweza kubadilisha mwelekeo wa siasa za Hungary na hata kuathiri uhusiano wake na mataifa ya Magharibi.