Papa ajizuwia kuzungumzia kashfa ya mapadri | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 05.04.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Papa ajizuwia kuzungumzia kashfa ya mapadri

Kardinali Sodano asema watu wa Mungu wako pamoja na Papa

default

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu, Benedict XVI.

Wakristo duniani kote wanaendelea na  maadhimisho ya sikukuu ya pasaka leo ikiwa ni Jumatatu ya Pasaka. Jana Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita aliongoza Ibada ya Misa ya Sikukuu ya Pasaka bila kuzungumzia chochote kuhusu kashfa za mapadri wa Kanisa hilo kuwanyanyasa watoto kingono zinalolitikisa Kanisa Katoliki sehemu mbalimbali duniani.

''Nawatakia nyote heri ya Pasaka. Amani na Baraka za Bwana ziwe kwenu nyote.''

Hivyo ndivyo Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita alivyokuwa akitoa salamu zake za sikukuu ya Pasaka.

Rom nimmt Abschied

Maelfu ya waumini waliokusanyika katika uwanja wa mtakatifu Petro mjini Roma.

Katika mahubiri yake kwenye Ibada hiyo ya Misa Baba Mtakatifu anayewaongoza Wakatoliki bilioni moja ulimwenguni kote, alilaani vitendo vya kuteswa na kunyanyaswa Wakristo wachache nchini Iraq na Pakistan, lakini alishindwa kuzungumzia tuhuma zinazolikabili kanisa hilo za mapadri wake kuwanyanyasa watoto kingono. Hata hivyo, Mkuu wa Makardinali, Mwadhama Angelo Kardinali Sodano alimkumbatia Baba Mtakatifu huku akimwambia kuwa watu wa Mungu wako pamoja naye na kwamba wasiruhusu wala kujali maneno ya uzushi ndani ya Kanisa Katoliki kwa sasa.

Nchini Ufaransa, Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini humo, Mwadhama Andre Kardinali Vingt-Trois, ameshutumu kampeni zenye lengo la kumchafua Baba Mtakatifu, kwamba alishindwa kushughulikia visa hivyo pindi alipokuwa Askofu Mkuu nchini Ujerumani. Kardinali huyo amesema kuwa ni Baba Mtakatifu ambaye kwa wakati huo alikuwa Kardinali Ratzinger na Mkuu wa Baraza la Kipapa la Imani, aliwasihi maaskofu kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya kuwanyanyasa watoto kingono ikiwemo kuiarifu Roma kuhusu visa hivyo.

Maaskofu kadhaa walaani vitendo hivyo

Lakini maaskofu wa ngazi za juu wa Ubelgiji na Ujerumani wamelaani hatua ya Kanisa Katoliki ya kuwalinda mapadri waliohusika na vitendo hivyo. Katika mahubiri yake ya Pasaka, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mechelen-Brussels, Mhashamu Andre Joseph Leonard alisema Kanisa halikushughulikia visa hivyo ipasavyo huku likikaa kimya. Naye Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani, Askofu Mkuu Robert Zollitsch alisema siku ya Pasaka ni siku maalum ya kutathmini mabaya yote yanayolikumba Kanisa hilo.

Katika hatua nyingine viongozi wa Kanisa wa Uingereza na Ireland wanajaribu kupooza machungu baada ya kiongozi wa Kanisa la Anglikana duniani, Askofu Mkuu wa Cantebury Rowan Williams kusema kuwa Kanisa Katoliki linapoteza uaminifu wake huko Ireland kufuatia kanisa hilo kuwalinda mapadri wanaotuhumiwa kuhusika na kuwanyanyasa watoto kingono. Aidha, Askofu mstaafu wa Jimbo la Evreux nchini Ufaransa, Mhashamu Jacques Gaillot amesema leo kuwa walifanya makosa kumkubali katika jimbo hilo padri wa Canada aliyekuwa akituhumiwa kuwanyanyasa watoto kingono katika miaka ya 1980. Askofu Gaillot ameongeza kuwa hivyo ndivyo Kanisa lilivyokuwa linafanya kazi kwa wakati huo. Askofu huyo alisema walikuwa wakitoa msaada kwani waliombwa kumchukua padri huyo asiyetakiwa na walikubali.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 05.04.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MnOW
 • Tarehe 05.04.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MnOW
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com