Obama na McCain wameahidi enzi mpya ya mageuzi | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.11.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama na McCain wameahidi enzi mpya ya mageuzi

Rais-mteule wa Marekani Barack Obama na mshindani wake wa Republikan alieshindwa John McCain wameahidi enzi mpya ya mageuzi kutenzua mzozo wa uchumi wa Marekani,kurekibisha sera ya nishati na kuhifadhi usalama wa taifa.

President-elect Barack Obama, right, meets with Sen John McCain, R-Ariz., Monday, Nov. 17, 2008, at Obama's transition office in downtown Chicago. (AP Photo/Pablo Martinez Monsivais)

Rais-mteule Barack Obama(kulia)akikutana na Seneta John McCain katika ofisi ya mpito ya Obama mjini Chicago Nov.17,2008.

Viongozi hao,majuma mawili kufuatia uchaguzi wa Novemba 4,wametoa taarifa ya pamoja baada ya kukutana mjini Chicago wakisema kuwa Wamarekani wa vyama vyote wanawataka viongozi wao waungane na warekebishe mienendo mibovo ya Washington.

Mkutano uliodumu saa moja katika makao makuu ya mpito ya Barack Obama mjini Chicago umeipa uzito ahadi ya kuzungumza na wapinzani wa zamani,huku rais mteule huyo akitayarisha agenda ya miaka minne ijayo. Obama na McCain walizungumzia juu ya haja ya kuanzishwa enzi mpya ya mageuzi na kuachana na mivutano ya Washington ili kurejesha imani katika serikali na vile vile kuipatia kila familia ya Marekani inayojitahidi kufanya kazi,uwezo wa kuendesha maisha yao.

Viongozi hao wawili wamesema,wanatazamia kufanya kazi pamoja kukabiliana na changamoto kali kama kupata ufumbuzi wa mgogoro wa fedha,kuanzisha mradi mpya wa nishati na kulinda usalama wa taifa.Mkutano huo ulihudhuriwa pia na rafiki mkubwa wa McCain Seneta wa Kirepublikan Lindsey Graham na mbunge Rahm Emanuel aliechaguliwa na Obama kuwa Mkuu wa Ikulu ya Marekani-White House.

Kwa mujibu wa duru ya tume ya mpito,Obama hatokwenda umbali wa kumpa McCain wadhifa wa uwaziri katika serikali yake.Ingawa McCain katika hotuba aliyotoa baada ya kushindwa na Obama majuma mawili yaliyopita,aliahidi kufanya kazi na rais mpya,viongozi hao wawili wanatofautiana sana katika masuala muhimu kama vile njia ya kurekebisha uchumi na msimamo wa Obama kutaka kumaliza vita vya Iraq.Hata hivyo wataalamu wanasema,kuna mengi ya kujadiliwa kati ya Obama na Mrepublikan McCain ambae tangu miaka alikuwa hafuati msimamo wa chama chake cha kihafidhina katika baadhi ya masuala kama uhamiaji, mabadiliko ya hali ya hewa na mageuzi ya kimaadili.

Kwa upande mwingine Obama katika mahojiano yaliyotangazwa siku ya Jumapili na stesheni ya televisheni ya Marekani CBS,alisema kutakuwepo angalao Mrepublikan mmoja katika baraza lake la mawaziri,lakini hakutaka kueleza zaidi.Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Condoleezza Rice, siku ya Jumatatu alikutana na wakuu wa tume ya mpito ya wizara ya mambo ya nje ya Obama,lakini hakuna dalili kuwa aliombwa kushiriki katika serikali itakayoundwa na Rais-mteule Barack Obama.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com