Obama na Huckabee washinda hatua ya kwanza | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.01.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama na Huckabee washinda hatua ya kwanza

IOWA yaanaza kutoa sura ya hali itakavyokua katika uteuzi wa wagombea urais nchini Marekani

Kwa ushindi mkubwa katika hatua ya kwanza ya kinyanganyiro cha kuwania uteuzi wa kuwa wagombea wa kiti cha Urais katika uchaguzi wa Novemba nchini Marekani, kilichoanzia huko IOWA, Mdemocrat Barack Obama na Mrepublican Mike Huckabee wameibuka washindi wakiwaangusha wagombea wenzao. Hatua itakayofuata sasa ni kutafuta ridhaa ya wanachama wa vyama vyao katika jimbo la New Hampshire.

Barack Obama aliwaangusha wenzake wa chama chake cha Democrats akimuacha John Edwards nafasi ya pili na Hilary Clinton mke war ais wa zamani Bill Clinton katika nafasi ya tatu. Hadi matokeo yanatangazwa Obama na Clinton ndiyo waliokua wakitajwa kuwa na ushindani mkubwa huku matumaini ya kuibuka mshindi yakielekezwa kwa bibi Clinton.

Ushindi wa Obama huko IOWA ni hatua ya kwanza katika kiu chake cha kutaka kuwa Rais wa kwanza mweusi katika historia ya Marekani na ametoa changa moto kubwa kwa wapinzani wake wakuu Edwards na Hilary Clinton, kutafakari juu ya mkakati wa kampeni zao kukiwa kumesalia maeneo mengine 28 ya kutafuta ridhaa ya wanachama, kabla ya kuidhinishwa na mkutano mkuu wa chama kuwa mgombea.

Kwa upande wa Warepublican Huckabee, gavana wa zamani wa Arkansas alimpa pigo mpinzani wake mkuu Mitt Romney, gavana wa zamani wa Massachussets, wakati John McCain akifuata katika nafasi ya tatu, lakini wachambuzi wanasema bado anakabiliwa na kazi ngumu huko New Hampshire.

Kwa sasa washindi wote wawili wa hatua hii ya kwanza Obama mwenye umri wa miaka 46 na Huckabee miaka 52 wamezusha mshtuko, wakati hapo kabla wakionekana kuwa nyuma ya wapinzani wao wakuu, kwa mujibu wa kura za maoni ya wanacahama wa vyama vyao.

Kampeni hii ya 2008 inatajwa kuwa ya uwazi kabisa kuwahi kuonekana katika kinyanganyiro cha kuwania uteuzi wa wagombea Urais katika kipindi cha miaka 50 iliopita, na ushindani huko IOWA unatajwa pia kuwa mkali kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Marekani.

Walioshiriki miongoni mwa Wademocrats walifikia 220.000 na kuivunja rekodi ya 2004 waliposhiriki wanachama 124.000. Hali hii inadhihirisha shauku kubwa walio nayo kuelekea uchaguzi wa Urais mwezi Novemba.

Kwa jumla wakati safari hadi ueuzi wa vyama vyao bado ni ndefu wapinzani wa Obama , Edwards na bibi Clinton kila mmoja anajiwekea matumaini na kwa wagombea wa Republican meya wa zamani wa New york Ruddy Giuliani ambaye hakukitilia manani sana kinyanganyro cha IOWA, anasema bado anaamini ana nafasi kubwa ya kuwa mgombea mteule wa chama chake.

Giuliani alikua jimboni Florida katika sehemu ya mkakati wa kujiimarisha katika maeneo ambayo wasaidizi wake wanasema ni muhimu zaidi katika kampeni yao.

 • Tarehe 04.01.2008
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CkCp
 • Tarehe 04.01.2008
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CkCp
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com