1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuingia makubaliano na Urusi?

Lilian Mtono
2 Februari 2022

Gazeti moja la nchini Uhispania hii leo limechapisha nyaraka zilizovuja zinazosema Marekani huenda ikawa tayari kuingia kwenye makubaliano na Urusi ili kupunguza mivutano baina yao.

https://p.dw.com/p/46QC2
Joe Biden
Picha: John Rucosky/The Tribune-Democrat/AP/picture alliance

Mivutano hiyo inatokana na hatua ya Marekani ya kuweka mifumo ya makombora Ulaya, lakini tu iwapo Moscow itakubali kuachana na chokochoko dhidi ya Ukraine. 

Katika toleo la leo Jumatano, gazeti hilo la El Pais limechapisha nyaraka mbili za Marekani zilizokuwa na muhuri wa "siri" zinazodai kwamba ni majibu ya kimaandishi ya Marekani na NATO kwa Urusi. Kulingana na gazeti hilo miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuwepo na mpangilio mpya wa kiusalama barani Ulaya.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani haikupatikana mara moja kuzungumzia ukweli wa taarifa hiyo na NATO pia imesema haiwezi kutoa tamko lolote.

Waraka huo umechapishwa siku moja baada ya rais wa Urusi Vadimir Putin kutuhumu mataifa magharibi kupuuza masharti muhimu ya kiusalama ya Urusi katika juhudi za kidiplomasia za kupunguza mzozo huo unaosambaa pamoja na hofu ya vita na Ukraine.

Urusi nayo haijazungumzia chochote kwa kuthibitisha ama kukanusha kuhusiana na taarifa hizo zilizovuja, lakini msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema tu kwamba wao hawajavujisha chochote.

Soma Zaidi: Baraza la Usalama kujadili mzozo wa Urusi na Ukraine

Niederlande I Kabinett unter Premier Mark Rutte I König vereidigt neue Regierung
Waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte ameahidi msaada wa kiteknolojia kwa Ukraine kujilinda na mashambulizi ya kimtandao.Picha: Sem van der Wal/AFP/Getty Images

Katika hatua nyingine, Uholanzi inaangazia iwapo itaweza kuisaidia Ukraine wataalamu wa masuala ya ulinzi wa mitandao katikatika ya juhudi za kidiplomasia za kupunguza mzozo na Urusi.

Waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte ambaye hii leo amemtembelea rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa ajili ya mazungumzo yaliyopangwa kwa muda mrefu kuhusiana na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi amesema majadiliano yao yalijikita katika wasiwasi uliopo kwa sasa katika mpaka wa Ukraine na Urusi.

Amesema namna pekee ya kupata suluhu kwenye mzozo huo ni Urusi kuondoa wanajeshi wake, diplomasia na majadiliano na kuongeza kuwa Uholanzi kwa sasa itaisaidia Ukraine kwa namna itakavyoweza ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kukabiliana na mashambulizi ya kimtandao dhidi ya Ukraine.

Ikumbukwe Urusi iliwahi kuishambulia Ukraine kimtandao na huenda ikafanya hivyo mara nyingine kama sehemu ya operesheni zake dhidi ya jirani yake.

Aidha taarifa za hivi karibuni zimesema wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon inataraji kutangaza hii leo kuwapeleka wanajeshi wake katika siku chache zijazo, baada ya rais Joe Biden kuidhinisha rasmi kuongezwa kwa idadi ya wanajeshi mashariki mwa Ulaya, hii ikiwa ni kulingana na maafisa waliozungumza na shirika la habari la Reuters.

Biden ameagiza kupelekwa kwa wanajeshi zaidi ya 3,000 ili kuimarisha nguvu ya washirika wake wa Ulaya, limeripoti gazeti la Wall Street Journal.

Mashirika:RTRE