1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin aishutumu Marekani na washirika wake kuipuuza Urusi

Sylvia Mwehozi
2 Februari 2022

Rais Vladmir Putin ameishutumu Marekani na washirika wake kwa kupuuza matakwa ya Urusi ya wasiwasi mkubwa wa kiusalama lakini akasema Moscow iko tayari kwa mazungumzo zaidi ili kupunguza mvutano.

https://p.dw.com/p/46OYl
Russland | PK | Treffen Putin und Orban in Moskau
Picha: Yuri Kochetkov/AP Photo/picture alliance

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Moscow sambamba na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, Putin amesema Urusi bado inaendelea kutathmini jinsi Marekani na Jumuiya ya kujihami NATO inavyoshughulikia matakwa ya kiusalama iliyoyatoa wiki iliyopita. Lakini ameongeza kuwa ni wazi nchi za magharibi zimepuuza matakwa ya Urusi ya NATO kutojitanua hadi Ukraine na mataifa mengine ya zamani ya Umoja wa Kisovieti.

"Hatujaona uzingatiaji wa kutosha wa matakwa yetu matatu muhimu kuhusu kuzuia upanuzi wa NATO, kukataa kupeleka vifaa vya kushambulia karibu na mipaka ya Urusi, na kurudisha miundombinu ya kijeshi ya Umoja huo barani Ulaya wa hali ilivyokuwa mwaka 1997" amesema rais Putin. 

Urusi: Majibu ya Marekani kuhusu Ukraine hayaridhishi

Aidha, Rais Putin ameelezea uwezekano wa hali ya baadaye ambapo Ukraine ikikubaliwa kuwa mwanachama wa NATO inaweza kutumia nafasi yake kujaribu kuitwaa tena rasi ya Crimea, eneo ambalo Urusi ililinyakua mwaka 2014. Amesema Washington kimsingi haijali usalama wa Ukraine bali inataka kukabiliana na Urusi, akisema Ukraine inatumika tu kama chambo kufikia lengo lake.

Ukraine Kiew | Besuch Boris Johnson, Premierminister Großbritannien | mit Wolodymyr Selenskyj, Präsident
Waziri Mkuu Boris Johnson na rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyyPicha: Peter Nicholls/AP Photo/picture alliance

Putin hajazungumza hadharani kuhusu mzozo wa Ukraine tangu Desemba 23, akiacha sintofahamu kuhusu nafasi yake binafsi wakati wanadiplomasia kutoka Urusi na nchi za Magharibi wamekuwa wakijishughulisha mara kwa mara na duru za mazungumzo. Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, ambaye mara nyingi amezozana na viongozi wenzake wa Ulaya juu ya demokrasia katika nchi yake, alisema kuwa anaamini baada ya mazungumzo yake na Putin bado kuna nafasi ya maelewano.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov na mwenzake wa Marekani Antony Blinken walizungumza siku ya Jumanne na kurejelea misimamo ya viongozi wao. Ikulu ya Marekani White House imesema kuwa marais hao wawili wanaweza kufanya mazungumzo mara tu Washington itakapopata mrejesho kutoka Moscow.

Kwa upande mwingine waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameendelea na juhudi za kidiplomasia wakati alipozuru Kiev kwa mazungumzo na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy. Johnson amemueleza Zelenskyy kuwa Uingereza inazo hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na vikwazo endapo kutakuwa na uvamizi. Johnson anatarajia kumpigia simu Putin leo Jumatano.

Kwa upande wake rais Zelenskyy amesema kiasi ya wanajeshi 100,000 wa Urusi wamekusanyika karibu na mpaka na nchi yake, wengine 35,000 hadi 50,000 wako Crimea na wengine wamepelekwa katika eneo la Ukraine linalodhibitiwa na waasi. Ameongeza kwamba wanachosubiri ni Urusi kuondoa wanajeshi wake na kwamba hiyo itakuwa ni ishara muhimu.

Vyanzo: AP/Reuters