Nini sababu za kifo cha kipa wa taifa Enke ? | Magazetini | DW | 12.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Nini sababu za kifo cha kipa wa taifa Enke ?

Hukumu ya Muuwaji wa mama wa kimisri -kifungo cha maisha.

Waislamu wakiandamana Dresden.

Waislamu wakiandamana Dresden.

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo, yametuwama takriban juu ya mada moja tu:kifo cha kuhuzunisha cha kipa wa Taifa na wa klabu ya Bundesliga ya Hannove 96, Robert Enke. Kuna wahariri wachache lakini,walioichambua hukumu ya jana ya kifungo cha maisha aliopitishiwa muuaji mama mjamzito wa kimisri kutokana na chuki tu za kikabila.

Gazeti la Osnabrücker Zeitung juu ya mada hii ya pili laandika:

"Yafurahisha kuona, hukumu aliopitisha hakimu wa Mahkama ya Dresden, ilikuwa wazi.Mjerumani huyo alihukumiwa adhabu ya juu kabisa ya kifungo cha maisha korokoroni kwa kumuua mwanamke wa kimisri mwenye-mimba mahkamani,mbele ya mwanawe na mumewe.Ulimwengu wa magharibi na ule wa kiarabu ,unatofautiana katika mengi,lakini una maadili ya aina moja ."

Ndio maana -linasema gazeti, kisa hiki kinatuzindua kupambana kwa ukali zaidi na wafuasi wenye siasa kali za chuki wa mrengo wa kulia miongoni mwa wajerumani.

Wakati huo huo lakini,laonya gazeti:

"Nguvu zichukuliwe tangu Misri hata kwengineko, kupambana na wale wanaotaka kuutumia uhalifu uliopita kuchochea na kupalilia chuki dhidi ya nchi za magharibi.Kwa ufupi,wachochezi wa ukabila bila kujali uraia na asili zao na hata dini zao,popote walipo wapigwe vita."

Tukigeukia kujiua kwa kipa wa Taifa wa Ujerumani, Robert Enke,gazeti la Saarbrücker Zeitung, laandika:

"Kwa ulimwengu mzima wa michezo nchini Ujerumani na hasa ule wa dimba,kifo cha Enkes ni pigo kubwa ambalo litaacha athari zake.Kwani, kinamuruka na kuanika tena dhahiri-shahiri , umuhimu usiofaa kutiwa maanani sana wa (show-business) katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani-Ligi ambayo mastadi wa kweli na wa uongo,vyombo vya habari na wanabiashara wanacheza dimba ili kunyakua sehemu yao katika soko la mabilioni ya fedha."

Gazeti linaongeza kusema kwamba, hata ingawa hakuna mafungamano ya moja kwa moja:

"Kushindwa kunako sikitisha marehemu Robert Enke kukabiliana na mitihani na changamoto za maisha na za kazi yake ya kucheza dimba,kunaanika hadharani kinyan'ganyiro kikali ,kisicho na huruma na kisichoruhusu udhaifu au unyonge."

Ama gazeti la jiji la Hannover:Allgemeine Zeitung laandika kwamba, mke wa marehemu Robert Enke, bibi Teresa, alijaribu jana mbele ya umati wa watu kuelezea hali isioelezeka. Laandika:

"Sio tu aliwasaidia watu wengi waliofadhahika kuelewa sababu kwanini, stadi wa dimba kipenzi cha mashabiki wengi,hakutaka kuishi tena. Akiugua maradhi ya fikra na hofu nyingi ambayo sio tu katika medani ya kispoti leo ni mwiko kuyazungumza,na alitaka kuyapa sura ya ubinadamu."

Likitukamilishia uchambuzi huu wa wahariri,gazeti la Flensburger Tageblatt,laandika:

"Kuhuzunika mno kwa familia ya wachezaji na mashabiki wa mpira katika kisa cha Robert Enke, kunafahamika.Kwani. marehemu alikuwa nyota mwenye moyo wa huruma,alieshughulikia mambo pia nje ya mpira.Pale nahodha wa timu ya Taifa ya Ujerumani Michael Ballack, alipoangua jana kilio mbele ya kamera za vyombo vya habari,Taifa zima la wachezaji na mashabiki wa dimba, lilia pia.Kuuvunja ule mpambano wa (Jumamosi ) hii dhidi ya Chile ,ni heshima ya mwisho kwa stadi wa dimba,ambae roho yake na kichwa chake, haikuijali tena heshima hiyo"

Mwandishi: Ramadhan Ali /DPA

Uhariri: M.Abdul-Rahman