1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUganda

Nchi wazalishaji kahawa Afrika zajadili thamani ya zao hilo

8 Agosti 2023

Viongozi wa mataifa 25 ya Afrika yanayozalisha kahawa wameazimia kuweka mikakati inayolenga kuchakata zao hilo ili bara linufaike zaidi kutokana na biashara hiyo.

https://p.dw.com/p/4UvFr
Kahawa | Kericho
Mkulima wa kahawa wa KenyaPicha: Billy Mutai/ZUMAPRESS/picture alliance

Kulingana na viongozi hao, mataifa ambayo hununua zao hilo likiwa katika kiwango cha malighafi hunufaika kwa asilimia 99 katika soko dola bilioni 460 la bidhaa hiyo duniani ambapo Afrika huingiza tu kipato cha dola bilioni 2.5 tu.

Kenya-Kahawa | Kericho
Kahawa mbichi iliyovunwa huko Kericho KenyaPicha: Billy Mutai/ZUMAPRESS/picture alliance

Akifungua rasmi kongamano la awamu ya pili la shirikisho  la Afrika la kahawa IACO, rais Yoweri Museveni wa Uganda ametoa angalizo kwamba ni jambo la kusikitisha kuwa mataifa ya Ulaya na Marekani  ambayo hununua na kuchakata  kahawa ndiyo hunufaika zaidi kuliko yale ambayo wakulima wake huzalisha zao hilo. Ameitaja hali hiyo kuwa mwenendo wa kuifyonza Afrika raslimali yake akisema.

Mkakati unaopendekezwa sasa ni kuona kwamba mataifa 25 ya Afrika  yanayozalisha zao hilo yanalichakata na kuliuza kama bidhaa tayari kwa watumiaji. Kwa namna hii Afrika itaingiza mapato zaidi na pia kubuni nafasi zaidi za kazi kwa wanawake na vijana. Rais wa Ethiopia Sahle- Work Zewde ameongezea kuwa pana haja ya madalali wa kahawa kutoka Afrika kunadi bidhaa hiyo kwa bei stahiki pamoja na kuwahimiza Waafrika kunywa kahawa zaidi kama ilivyo katika nchi yake.

Baraza za Kahawa

Asilimia 50 ya kahawa inayozalishwa Ethiopia hununuliwa na wenyeji ikilinganisha na mataifa kama Uganda ambapo mauzo ya bidhaa hiyo ndani ya nchi ni chini ya asli mia 10. Amesema.

Kwa upande wake makamu wa rais wa Tanzania Phillip Isdore Mpango amefafanua kuhusu mikakati mbalimbali inayolenga kuboresha na kuzidisha uzalishaji wa zao hilo ili wakulima wanufaike zaidi na pia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha Tanzania ambayo ndiyo itakuwa mwenyeji wa kongamano hilo mwaka ujao ina mikakati ya kuendesha mafunzo maalumu kujenga uwezo wa wajasiriamali katika mnyororo wote wa kuzidisha thamani ya zao  hilo. Waziri mkuu wa Kenya Musalia Mudavadi ameorodhesha manufaa ya zao la kahawa kwa nchi hiyo ikiwemo kupunguza umasikini na kuhakikisha kuwepo kwa chakula cha kutosha kwa zaidi ya wakenya milioni 5 wanaotegemea zao hilo moja kwa moja au kwa namna mbalimbali za mnyororo wa biashara hiyo.