″Nafasi ya mwisho kwa binadamu″ | Magazetini | DW | 19.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

"Nafasi ya mwisho kwa binadamu"

Adapt: Maja Dreyer 102640 Jumatatu hii, wahariri wanayatathmini matokeo ya mwishoni mwa wiki ambayo mara hii hasa ni onyo la wataalamu wa halmashauri ya kimataifa inayojihusisha na hali ya hewa.

Lini utoaji wa gesi chafu utapunguzwa?

Lini utoaji wa gesi chafu utapunguzwa?

Katika ripoti yao iliyotolewa baada ya mkutano wao wa wiki nzima huko Valencia, Spain, wataalamu hao wanachora picha mbaya ya siku za usoni na kutoa mwito kuchukuliwa hatua kali kuzuia ongezeko zaidi la ujoto duniani. Kwanza ni gazeti la “Kölnische Rundschau” ambalo limeandika hivi: “Hiyo ni nafasi ya mwisho kwa binadamu: Kila mmoja wetu anapaswa kufahamu uzito wa maonyo haya. Muda wa kugombana juu ya faida ya kutunza hali ya hewa umekwisha sasa. Hakuna maneno bora zaidi kama yale yaliyotumiwa na wataalamu hao wao halmashauri ya kimataifa kueleza juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na kusema kwamba bado kuna fursa ya kupambana na changamoto hiyo.”

Mhariri wa “Westfälische Rundschau” lakini, licha ya uzito wa ripoti hiyo mpya, ana wasiwasi kwamba nchi fulani muhimu hazikubali kuhusika katika suala hili. Ameandika: “Licha ya kwamba hatuwezi tena kuficha uzito wa hali ilivyo, bado wale wanaochangia zaidi katika kusababisha kupanda kwa joto wanakataa kubeba dhamana na kuchukua hatua zinazohitajika. Marekani kwa mfano inazinyoshea kidole nchi nyingine na bado haijatia saina makubaliano ya Kyoto kuhusu kupunguza utoaji wa gesi chafu. Hivyo, Rais Bush anazipa uwanja nchi nyingine zinazoendelea haraka kiuchumi kama vile China na India kutofanya chochote.”

Ripoti hiyo ya wataalamu wa hali ya hewa kutoka kila pembe ya dunia itatumika kama msingi wa mkutano wa kilele kuhusu utunzaji wa hali ya hewa utakaofanyika huko Bali, Indonesia mwezi wa Disemba mwaka huu. Mhariri wa “Märkische Oderzeitung” lakini hana matumaini kubwa kwamba mkutano huu utaleta matokeo ya maana, kwa sababu: “Inaonekama kama Marekani tayari inajiandaa kuwa kama breki ya mkutano huu na kuzuia makubaliano makubwa. Ikiwa ni hivyo, matarajio kweli ni mabaya. Kwa sababu mkutano huu unabidi kuwa na matokeo yenye uzito na siyo makubaliano yasiyo na maana. Bila ya kujiwekea masharti, hatutaweza kuzuia misiba na maafa yaliyokaridiwa na wataalamu wa hali ya hewa.”

Na la mwisho ni gazeti la “Frankfurter Allgemeine”. Uchambuzi wake ni ufuatao: “Kimsingi, ripoti hiyo mpya inaonyesha kwamba makubaliano ya Kyoto yamepoteza umuhimu wake. Hata wataalamu wa halmashauri ya kimataifa hawakutaka kuungama haya kwa sababu inatoa picha kama sera za utunzaji wa hali ya hewa zimeshindwa. Ukweli wa mambo ni kwamba, utoaji wa gesi chafu haujapunguzwa katika miaka iliyopita kama ilivyoamuliwa huko Kyoto, bali umeongezeka mara mbili. Katika hotuba yake hapo Jumamosi, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon hakusisitiza tu kundi hili la nchi zilizotia saini makubaliano ya Kyoto lakini aliwataja watoaji wakuu wa gesi chafu, Marekani na China, jukumu kubwa katika ulinzi wa hali ya hewa.”

 • Tarehe 19.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CJBw
 • Tarehe 19.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CJBw