Nadya akiri makosa ya kumuambikiza mpenzi wake virusi vya HIV | Masuala ya Jamii | DW | 16.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Nadya akiri makosa ya kumuambikiza mpenzi wake virusi vya HIV

Muimbaji mashuhuri wa Ujerumani, Nadja Benaissa, amefikishwa mbele ya mahakama ya mjini Darmstadt kujibu mashtaka ya kumuambukiza mwanamume mmoja, virusi vya HIV, kwa kufanya naye bila kinga

Wakati wa kuanza kusikilizwa kesi hiyo mjini Darmstadt, Nadya mwenye umri wa miaka 28 aliungama makosa yake kwa kusababisha hatari kwa maisha ya wanaume hao aliofanya nao mapenzi kati ya mwaka 2000 na 2004. Mmoja kati ya wapenzi wake aliambukizwa ukimwi, huku wengine wawili wakaepuka kupata virusi vya HIV, vinavyosababisha ugonjwa huo. Kwa mujibu wa waongoza mashataka wa serikali, Nadja aligundua ana virusi vya HIV mnamo mwaka 1999. Msemaji wa mahakama hiyo ya mjini Darmstadt, magharibi mwa Ujerumani amesema Nadja amekiri kufanya mapenzi bila kutumia kinga muda mfupi baada ya kesi yake kuanza kusilikilizwa katika mahakama hiyo.

Mwanamume aliyeambukizwa virusi ambaye jina lake haliwezi kutajwa kwa sababu za kisheria amesema maisha yake yameharibiwa sana. Nadja amenukuliwa na jarida la kila wiki la hapa Ujerumani la Stern, akisema na hapa namnukulu, "Naomba radhi kutoka moyoni mwangu. Jambo la mwisho ambalo nililitaka ni mpenzi wangu aambukizwe virusi vya HIV," mwisho wa kumnukulu. Amelia kwa uchungu huku machozi yakimtiririka na kukiri kwamba alijaribu kupuuzilia mbali ukweli kwamba alikuwa anaishi na virusi vya HIV na alikuwa amepoteza mwelekeo na kushindwa kuyadhibiti maisha yake wakati huo.

Msichana huyo mzaliwa wa mji wa Frankfurt, mamake Mjerumani na babake Mmoroko, aliasisi bendi maarufu ya humu nchini ijulikanayo kwa jina No Angel, mnamo mwaka 2000. Bendi hiyo ndiyo bendi ya wasichana iliyofanikiwa zaidi hapa Ujerumani. "Nilishindwa nguvu na ufanisi wa bendi yetu na kupigwa na butwaa na matokeo ya uchunguzi niliofanyiwa yaliyobaini kuwa nina virusi. Sikuweza kumwambia mtu yeyote. Niliogopa sana," ameongeza kusema Nadja mbele ya mahakama ya mjini Darmstadt.

Nadja Benaissa alitiwa mbaroni kwa mara ya kwanza mwezi Aprili mwaka jana, wakati alipokuwa akijiandaa kutumbuiza katika klabu moja mjini Frankfurt na kuzuiliwa kwa siku 10. Muimbaji huyo mwenye mtoto wa kike wa umri wa miaka 11, hajaanza kupata dalili za ukimwi.

Hatua ya waongoza mashtaka kuchapisha taarifa yake kuhusu hali yake ya afya ilizusha ukosoaji mkubwa kwamba mrembo huyo hakutendewa haki. Nadja anakabiliwa na kifungo cha kati ya miezi sita hadi miaka 10 jela iwapo atapatikana na hatia. Kesi yake inatarajiwa kuendelea kusikiliwa kwa siku nne zijazo. Wanachama wenzake wa bendi ya No Angel, akiwemo Sandy Moelling, Jessica Wahls na Lucy Diakovska, pia wanatarajiwa kushuhudia mbele ya mahaka ya mjini Darmstadt. Kesi hiyo inasilikilizwa na mahakimu wa mahaka ya watoto kwa sababu Nadja alikuwa na umri wa miaka 17 wakati inapodaiwa alifanya mapenzi bila kutumia kinga mnamo mwaka 2000.

Mwandishi: Josephat Charo/DPAE

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 16.08.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OorX
 • Tarehe 16.08.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OorX
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com