1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakubali kimsingi kupelekewa uranium?

Abdu Said Mtullya22 Oktoba 2009

Mswada wa makubaliano juu ya kuipa Iran uranium iliyorutubishwa wafikiwa mjini Vienna.

https://p.dw.com/p/KCbf
Mkurugenzi wa shirika la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia duniani, Mohammed Elbaradei.Picha: picture-alliance / dpa


Baada ya mazungumzo ya siku tatu, mjini Vienna ,Iran,Urusi, Marekani na Ufaransa zimefikia mswada wa makubaliano juu ya kuipelekea Iran madini ya Uranium yaliyo rutubishwa kabisa.Mswada huo unatarajiwa kuidhinishwa kesho.

Mkuregenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalodhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia,IAEA Mohammed Elbaradei ameuwasilisha mswada huo mjini Vienna ambao amesema unazingatia maslahi ya pande zote.

Bwana Elbaradei ameeleza kuwa hati hiyo inaonyesha jinsi ya kusonga mbele.Pande zinazohusika zitatoa jibu hapo kesho iwapo zitaiidhinisha hati hiyo.

Mswada huo ni juu ya kuipelekea Iran madini ya uranium yaliyokwisharutubishwa.

Kuanzia jumatatu, wajumbe wa Iran na wa Urusi, Marekani na Ufaransa wamekuwa wanajadili pendekezo juu ya kuipatia Iran uranium ambayo haiwezi kutumika kwa ajili ya kuundia silaha za nyuklia.

Lakini Iran imesema wazi kuwa haitaki Ufaransa iwe sehemu ya mradi huo.

Nchi za magharibi zinakusudia kuudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran kwa kiwango kikubwa kutokana na kuhofia kwamba nchi hiyo inalenga shabaha ya kuunda silaha za nyuklia.

Mswada uliofikiwa unaonyesha mabadliko katika msimamo wa Iran. Hapo awali rais Mahmoud Ahmadinejad aliziambia nchi za magharibi kwamba zisifikirie zinacheza na mtoto wa miaka minne zinapozungumza na Iran.

Lakini mswada wa makubaliano uliotolewa mjini Vienna kimsingi unaashiria kuwa Iran ipo tayari kukubali pendekezo juu ya kupelekewa madini ya uranium yaliyokwisharutubishwa.Iran imesema tu kwamba haitaki Ufaransa ishiriki katika mradi huo.

Urusi, Ufaransa na Marekani zimekuwa zinaitaka Iran ikubali haraka mapatano yaliyofikiwa mjini Geneva tarehe mosi mwezi oktoba.

Kwa mujibu wa mapatano hayo Iran itapeleka nchini Urusi ,kilogramu 1200 za uranium yake, ili irutubishwe na halafu ipelekwe Ufaransa mwishoni mwa mwaka.

Lakini mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalodhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia IAEA ,Mohammed Elbaradei hakusema iwapo Iran imekubali pendekezo hilo.

Lakini kiongozi wa ujumbe wa Iran Ali Asghar amesema tu kwamba nchi yake itapatiwa nyenzo kwa ajili ya kinu chake cha utafiti kinachokidhi mahitaji kwa manufaa ya tiba ya saratani.-Bwana Ali Asghar amesema Iran itatoa habari kamili hapo ijumaa.

Mwandishi/Mtullya Abdu. AFPE/ZA

Mhariri/Abdul-Rahman