1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa sera ya nje ya Umoja wa Ulaya ziarani Uturuki

Saleh Mwanamilongo
3 Machi 2020

Mkuu wa sera ya nje na usalama wa Umoja wa Ulaya,Josep Borrel anatarajiwa kuwasili mjini Ankara leo kwa ziara ya siku mbili nchini Uturuki, ambako atakukutana na rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdongan kuzungumzia Syria

https://p.dw.com/p/3YnOL
Josep Borrel, mkuu wa sera za nje na usalama wa umoja wa ulaya
Josep Borrel, mkuu wa sera za nje na usalama wa umoja wa ulayaPicha: Imago Images

Mkuu wa sera ya nje na usalama wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrel anatarajiwa kuwasili mjini Ankara leo kwa ziara ya siku mbili nchini Uturuki, ambako atakukutana na rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdongan kuzungumzia mzozo wa wahamiaji na wakimbizi wa Syria. Rais wa Uturuki amesema leo kwamba Umoja wa Ulaya haujatekeleza majukumu yake ya mkataba wakimbizi na wahamiaji walioko nchini Uturuki. 

Mazungumzo hayo yanaelezewa na Umoja wa Ulaya kuwa ni ya ngazi ya juu baina Josep Borrel na rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kuhusu hali ya jimbo la Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria. Borrel anasindikizwa na kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na mizozo, Janez Lernarcic ambao watazungumza na viongozi wa Uturuki kuhusu madhara ya kiutu kwa raia wa Syria wanaozingirwa kwenye maeneo ya vita na vilevile hali ya wakimbizi wa Syria waliko Uturuki.

Mkutano huo wa viongozi wa EU umekuja kabla ya mkutano wa dharura wa mawaziri wa mamabo ya nje wa nchi za umoja huo, alkhamisi na ijumaa ijayo mjini Zagreb. Mkutano huo utakaoongozwa na bwana Borrel, utajikita zaidi juu ya hali ya Syria na tofauti baina ya uturuki na Umoja wa Ulaya.

 

Rais wa Uturuki atekeleza vitisho vyake

Kwenye mkutano wa pamoja na waziri mkuu wa Bulgaria Boyko Borisov,na wandishi habari mjini Ankara, rais wa Uturuki amesema kwamba EU imeendelea kuwa ndumila kuwili kuhusu suala la wakimbizi.

''Nilielezea miezi kadhaa iliopita kwamba ikiwa Umoja wa Ulaya hautuungi mkono kwa dhati kuhusu mzigo  huu wa pamoja, tutafunguwa mipaka'' alisema Erdogan.

 ''Tulikamilisha ahadi zetu kufuatia mkataba baina ya  EU na Uturuki. Katika hali hii, matarajio yetu kuhusu kugawa mgizo huu wa wakimbizi hayakupewa majibu. Hakuna mtu anahaki ya kuchezea heshma ya Uturuki'', aliendelea kusema rais wa Uturuki.

Ijumaa mkuu wa sera ya kigeni ya Umoja wa Ulaya ,Josep Borrel alielezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kuzuka mzozo mkubwa  wa kivita wa kimataifa nchini Syria. Kwa upande wake kamishna anayehusika na mizozo kwenye Umoja wa Ulaya Lenarcic atazuru kambi ya wakimbizi wa Syria ilioko Gaziantep, kusini mwa Uturuki.

Wakimbizi wa Syria kwenye mpaka baina ya Uturuki na Ugiriki
Wakimbizi wa Syria kwenye mpaka baina ya Uturuki na UgirikiPicha: Imago Images/Depo Photos/E. Corut

Viongozi wengine wa EU kutembelea Ugiriki

Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel na rais wa Halmashauri kuu ya  Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen watakwenda kwenye eneo la mpaka na Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis siku ya jumanne.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, serikali ya Ugiriki imesema, ''Uturuki, badala ya kupambana kuziba njia za wasafirishaji wa wahamiaji na wakimbizi, yenyewe ndio imekuwa msafirishaji.''

Ugiriki imezuia maombi mapya ya hifadhi kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao, kwasababu ya kile ilichokiita ''uratibu wa usafirishaji wa wahamiaji'' kutoka Uturuki.