1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Trump na Kim Jong Un kufanyika Hanoi

Grace Kabogo
9 Februari 2019

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema mkutano wake na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un utafanyika baadae mwezi huu, kwenye mji mkuu wa Vietnam, Hanoi.

https://p.dw.com/p/3D2j6
Bildergalerie Kim Trump
Picha: Reuters/J. Ernst

Trump ameandika leo katika ukurasa wake wa Twitter kwamba wawakilishi wake wameondoka Korea Kaskazini baada ya kufanya mazungumzo yaliyofanikiwa na wamekubaliana kuhusu muda na siku ya kufanyika kwa mkutano huo wa kilele kati yake na Kim.

Amesema mkutano huo wa pili kati ya viongozi hao utafanyika Februari 27 na 28. Trump na Kim walikutana kwa mara ya kwanza mwaka uliopita huko Singapore.

Korea Kaskazini na uchumi mkubwa

Trump amebainisha kuwa Korea Kaskazini chini ya uongozi wa Kim, itakuwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi. Kiongozi huyo wa Marekani amesema amejiandaa kukutana na Kim ili kuendeleza mchakato wa amani.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa mjumbe maalum wa Marekani nchini Korea Kaskazini, Stephen Biegun atakutana tena na maafisa wa Korea Kaskazini kabla ya mkutano wa Trump na Kim. Biegun amewasili Seoul, Korea Kusini akitokea Pyongyang baada ya kufanya ziara ya siku tatu ambako alijadiliana na maafisa wa Korea Kaskazini kuhusu mkutano wa viongozi hao.

USA Vertreter des Außenministers für Nordkorea Steve Biegun
mjumbe maalum wa Marekani nchini Korea Kaskazini, Stephen BiegunPicha: Getty ImagesAFP/N. Kamm

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imeeleza kuwa Biegun alijadiliana kuhusu nia ya Kim kuachana na silaha za nyuklia, kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Korea Kaskazini pamoja na kuweka amani ya kudumu katika Rasi ya Korea. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini, Noh Kyu-Duk amesema Biegun aliwasili jana Ijumaa usiku kwenye kambi ya anga ya Marekani ya Osan.

Biegun amesema kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kabla ya mkutano huo ujao. Kauli hiyo ameitoa leo wakati akimuarifu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini, Kang Kyung-Hwa kuhusu ziara yake ya Korea Kaskazini. '' Tuna kazi ngumu mbele yetu ya kufanya na serikali ya Korea Kaskazini. Nina uhakika kama pande zote mbili zinaendelea kuonesha nia, kweli tunaweza kupiga hatua kubwa,'' alisema Biegun.

Wataalamu wanasema suala la Korea Kaskazini kuhusu silaha za nyuklia linapaswa kuangaliwa kwa uzito na kupatiwa ufumbuzi yakinifu katika mkutano baina ya viongozi hao wawili na liachwe kupuuzwa kama jambo la mzaha.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP
Mhariri: Iddi Ssessanga