1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa juu ya HIV na Ukimwi waanza leo New York

Saumu Ramadhani Yusuf7 Juni 2011

<p>Viongozi wakuu wa dola na serikali duniani wanakutana hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kuzungumzia juu ya mpango wa matibabu dhidi ya maradhi ya Ukimwi na virusi vya Hiv.

https://p.dw.com/p/11W1d
Ufadhili wa miradi ya kupambana na Ukiwmi uliongezeka hadi dola bilioni 15.9 kwa mwaka kufikia 2009
Miongoni mwa viongozi watakaohudhuria mkutano huo wa kilele ni pamoja na marais wa Nigeria Jonathan Goodluck,rais wa Rwanda Paul Kagame na rais Ali Bongo wa Gabon.Shirika la kupambana na kuenea kwa maradhi hayo la Umoja wa Mataifa UNAIDS limeshatoa mwito wa kuwataka viongozi hao wa dunia kuwafikiria mamilioni ya watu wanaotegemea matibabu ya kupunguza makali virusi  vya HIV.

Mkutano huo wa kilele unaoanza leo unategemewa kupitisha uamuzi juu ya ni watu wangapi duniani watapata nafasi ya kupokea matibabu maalum ya kupunguza makali ya maradhi hayo yaliyokwisha sababisha vifo vya kiasi watu millioni 30 katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.

Kinder im Aids Hospiz in Addis Abeba
Watoto wenye virusi vya HIV na Ukimwi katika kituo cha kimisheni cha kuwasaidia nchini EthiopiaPicha: AP Photo

Viongozi wakuu 30 wa dola na serikali zitakazotoa fedha za kugharimia mpango huo watajadiliana kwa kina juu ya kiasi gani cha watu wanaostahili kupewa dawa na matibabu maalum ambayo kwa mujibu wa utafiti mpya imeonyesha ni utaratibu unaoweza kupunguza kwa kiwango kikubwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Kundi la madaktari wasiokuwa na mipaka la Medicins Sans Frontieres limeutaka mkutano huo kuwafikiria watu millioni 9 katika mpango huo wa matibabu ya Ukimwi katika kipindi cha miaka 4 ijayo pendekezo ambalo linakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wachangiaji kadhaa muhimu wa fedha katika mpango huo. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa watu millini 34 wanakadiriwa kuishi na virusi vya Ukimwi na wengine zaidi ya millioni 9 hawapati matibabu.

Wanadiplomasia wanasema kwamba majadiliano juu ya idadi ya wanaopaswa kupokea matibabu hayo katika nchi mbali mbali ambayo yanaweza kubadili kabisa gharama kwa mamilioni ya dolla yamekuwa yakiendelea tangu hata kabla ya mkutano wa leo.

Hata hivyo wataalamu na wanaharakati wa kupambana na maradhi ya Ukimwi wanasema kwamba itakuwa hakuna maana ikiwa nchi wafadhili wa mpango huo dhidi ya kuenea kwa Ukimwi hawatokuwa tayari kutoa fedha zinazohitajika  wakati kunahitajika hatua madhubuti za kungo'a kabisa shina la janga hilo.

Shirika la UNAIDS linasema kwamba kunahitajika billioni 6 zaidi kila mwaka kuepusha vifo vya watu millioni 7 kufikia mwaka 2020.Fedha hizo zitatumika kununua madawa yanayoweza kupunguza idadi ya kila mwaka ya maambukizi mapya kutoka watu millioni 2 .5 mwaka 2009 hadi watu millioni 1 kufikia mwaka 2015.

Aidha makundi ya wataalamu wa afya yanasema kwamba serikali za dunia zinabidi kuchukua hatua ya kupunguza gharama za madawa.

Mwandishi Saumu MwasimbaAFPE

Mhariri AbdulRahman.