Mkutano wa hali ya hewa waingia siku yake ya pili mjini Copenhagen | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 08.12.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mkutano wa hali ya hewa waingia siku yake ya pili mjini Copenhagen

Matumaini ya kufikiwa makubaliano yanazidi kupata nguvu baada ya shirika la Marekani EPA kukiri moshi wa viwandani unaathiri afya ya binaadam

default

Moshi unatoka katika viwanda vya mbolea vya Mumbai nchini India

Mkutano wa kimataifa kuhusu hali ya hewa umeingia katika siku yake ya pili hii leo mjini Copenhagen.Wakati huo huo mkutano huo wa Copenhagen umepata nguvu baada ya shirika la kuhifadhi mazingira nchini Marekani-EPA kukiri kwa mara ya kwanza kabisa kwamba moshi unaotoka viwandani unaathiri afya ya raia.

Majadiliano kuhusu hali ya hewa yaliyoanza kwa kutolewa kauli za matumaini mema jana mjini Copenhagen,yameingia katika awamu tete hii leo na hasa linapohusika suala la kugawana majukumu katika juhudi zisizoepukika za kupunguza moshi unaotoka viwandani.

Wawakilishi kutoka mataifa 193 wanakutana katika mji mkuu wa Danemark hadi December 18 ijayo kwa lengo la kufikia makubaliano ya kimataifa ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa-lengo kuu linaloungwa mkono na wote likiwa kupunguza moshi wa Carbon Dioxide unaotoka viwandani hadi kufikia kiwango cha Digree mbili za Celsius .

Kuanzia sasa wajumbe wameunda makundi kuratibu masuala yanayostahiki kuzingatiwa katika makubaliano hayo-ikiwa ni pamoja na hatua kadhaa za kiufundi mfano katika suala la jinsi ya kupambana dhidi ya kufyekwa misitu.Makundi hayo yanapaswa yakamilishe shughuli zao kabla ya mkutano wa mawaziri wa mazingira mwishoni mwa wiki hii,utakaofuatiwa na mkutano wa kilele December 17 ijayo.

Utaratibu wa muda mfupi na pia wa muda wa wastani wa kuzisaidia nchi zinazokabiliwa zaidi na balaa la mabadiliko ya hali ya hewa ni mojawapo ya mada tete mazungumzoni.

Ikiwa fikra ya awali ni kutenga dala bilioni kumi kwa mwaka hadi ifikapo mwaka 2010 inaonyesha kuungwa mkono,nchi zinazoinukia zinadai zipatiwe misaada mikubwa zaidi.

Kwa upande mwengine mashirika chungu nzima yasiyomilikiwa na serikali yanaendelea na harakati zao za kuwazinduwa watu majiani mjini Copenhagen na hata wajumbe katika ukumbi wa mkutano wa Bella Center.

Bella center Kopenhagen

Jengo la mkutano Bella center mjini Copenhagen

Tukio la kutia moyo limeripotiwa pia Marekani ambako shirika la ulinzi wa mazingira EPA,limechapisha ripoti inayoonyesha aina sita za moshi ikiwa ni pamoja na Carbon Dioxide unaathiri afya ya binaadam.

Mwenyekiti wa shirika hilo Lisa Jacksopn anasema:

""Tunafika katika mazungumzo ya hali ya hewa mjini Copenhagen tukiwa na dhamiri madhubuti za kukabiliana na mabadiliko.Tunataraji taarifa hii itasaidia kufikia makubaliano."

Mwenyekiti wa shirika hilo la ulinzi wa mazingira amesema hivi sasa shirika lake linaruhusiwa na linalazimika kuendeleza juhudi za kupunguza moshi unaochafua mazingira.

Zaidi kuliko hayo,ripoti hiyo inampa satua rais Barack Obama atekeleze ahadi alizotoa kabla ya kuelekea Copenhagen,ya kupunguza moshi wa Carbon Dioxide kwa asili mia 17 hadi ifikapo mwaka 2020,ikilinganishwa na mwaka 2005 hata bila ya ridhaa ya bunge la Congress.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir/ AFP

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 08.12.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KwcF
 • Tarehe 08.12.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KwcF
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com