Mkutano mkuu wa SPD wasema ″ndio″ | Magazetini | DW | 21.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Mkutano mkuu wa SPD wasema "ndio"

Mada moja tuu :Ridhaa iliyopatikana katika mkutano mkuu wa chama cha Social Democratic kuanzisha mazungumzo ya kuunda serikali pamoja na vyama ndugu vya Christian Democratic Union-CDU na Christian Social Union-CSU.

Maandamano yamefanyika sambamba na mkutano mkuu wa dharura wa SPD mjini Berlin

Maandamano yamefanyika sambamba na mkutano mkuu wa dharura wa SPD mjini Berlin

Mada moja tuu ndio iliyohanikiza magazetini hii leo:Ridhaa iliyopatikana katika mkutano mkuu wa chama cha Social Democratic kuanzishwa mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu pamoja na vyama ndugu vya Christian Democratic Union-CDU na Christian Social Union-CSU.

Tuanze basi na gazeti linalosomwa na wengi la Bild linaloandika:"Ruhusa ya kuanza mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano pamoja na vyama ndugu vya CDU/CSU,iliyotolewa na viongozi wa chama cha Social Democratic katika mkutano wao mkuu wa dharura ni uamuzi pekee wa busara!Kwasababu kura ya "La" kwa serikali hiyo ya muungano ingemaanisha kuzidi kukidhoofisha chama cha SPD kwa miaka kadhaa.Ni jukumu la SPD kuhakikisha maisha ya binaadam yanaimarika hata kama yanaimarika kidogo tu.Wakiachilia mbali jukumu hilo,watapoteza pia umuhimu wao.Wakishirikiana na vyama ndugu vya CDU/CSU,SPD watadhihirisha madai yao ya kutaka maisha bora kwa wananchi ni ya dhati.Na masharti ni mazuri:kutokana na makadirio mema ya ukuaji wa kiuchumi,mabilioni yanaweza kuwekezwa kwa mfano katika kuimarisaha hali shuleni na katika vituo vya kuwatunza watoto wadogo.Sawa sawa na vile ambavyo SPD daima wamekuwa wakipigania.Kunyanyua maisha ya jamii kupitia elimu ndio ahadi inayopigiwa upatu na SPD.Sasa kwa hivyo wanabidi waitekeleze."

SPD-Konvent Sigmar Gabriel

Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel akihutubia mkutano mkuu wa dharura wa chama chake

SPD wanatambua

Gazeti la mjini Dresden "Sächsische Zeitung" linahisi SPD wameutambua ukweli wa mambo.Gazeti linaendelea kuandika:"Yadhihirika kana kwamba vyama ndugu vya CDU/CSU na SPD tangu duru ya mwanzo ya mazungumzo ya kupima uwezekano wa kuunda serikali ya muungano vilitambua hali halisi namna ilivyo.Madai ya kuwepo kiwango jumla cha mshahara wa chini watalazimika SPD hivi sasa kuyapa umbele ili kufidia madai mengine ambayo pengine yatashindwa kutekelezwa.Na hata madai ya kiwango cha chini cha mshahara ni mbinu ya hatari,hasa kwa wakaazi wa majimbo ya mashariki ya Ujerumani ambao mshahara wao ni mdogo."

Merkel Gabriel Sondierungsgespräch

Kansela Angela Merkel wa chama cha CDU na Sigmar Gabriel wa SPD

Kugawana nyadhifa serikali

Baadhi ya wahariri wanaanza kuashiria wadhifa gani atakabidhiwa nani katika serikali kuu ya muungano wa vyama vikuu.Gazeti la "Der neue Tag" linaandika:"Licha ya kushindwa,milango yote ni wazi kwa Sigmar Gabriel.Anaweza kuwa makamo kansela:Sharti pekee ni kwamba katika mazungumzo pamoja na vyama ndugu vya CDU/CSU ,mwenyekiti huyo wa chama cha Social Democratic atabidi afikie makubaliano yatakayoungwa mkono na wengi katika chama chake cha SPD.Kwasababu watakaokuwa na usemi wa mwisho kuhusu makubaliano hayo ni wanachama 470 000 wa SPD na kwa namna hiyo wao ndio watakaoamua pia kuhusu mustakbal wa kisiasa wa wale waliofikia makubaliano hayo pamoja na CDU/CSU.Hilo Gabriel analitambua na ndio maana atalazimika kuendelea kutumia busara na kupima anachokisema ili kutowapa sababu wafuasi wao ya kujiwekea matumaini makubwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman