Mkutano juu ya Irak huko Sham el Sheikh | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano juu ya Irak huko Sham el Sheikh

Usalama nchini Irak utakua usoni kabisa katika ajenda ya mkutano wa wiki hii nchini Misri.Mvutano kati ya Iran na Marekani juu ya mradi wa nuklia huenda lakini ukautekanyara.

Iraq, iliovurugwa kwa machafuko na mauaji, inatumai mkutano wa kilele juu ya usalama unaofanyika wiki hii nchini Misri, na hasa kutoka nchi jirani, kukomesha umwagaji damu nchini mwake.Iraq, inahofia hatahivyo,kwamba mkutano huo unaweza ukatekwanyara na mazungumzo kati ya Marekani na Iran.

Tarehe 3 na 4 Mei,viongozi kutoka nchi jirani na Iraq ,wanachama 5 wa kudumu wa Baraza la Usalama la UM na kundi la nchi 8 tajiri watakutana huko Sham el Sheikh kuzungumzia machafuko nchini Iraq.

Mkutano huu lengo lake ni kusaka njia kuikomboa Irak kutoka machafuko yake ya hivi sasa yanayotishia kutapakaa nchi nyengine za ghuba na mwishoe, kugeuka mzozo wa eneo zima.

Kikao hiki na jaribio la pili linalofanywa na serikali ya Baghdad mnamo muda wa miezi 2 kuleta maridhiano na majirani zake –baadhi yao wanatuhumiwa kuchochea ghasia na kulishia silaha na wapiganaji nchini Iraq.

Bingwa mmmoja wa hali ya Iraq, Joost Hiltermann, amenukuliwa kusema,

“Ni muhimu sana kuona maendeleo yanafanyika katika kikao hiki kwavile hali ya Irak haiwezi kupatiwa ufumbuzi bila ya msaada wa majirani zake.” Mwisho wa kumnukulu.

Wakuu wa Iraq, wakijitahidi sana kuona mkutano huu unafanikiwa na uamuzi wa juzi jumapili wa Iran kuhudhuria kikao hiki, licha ya kuwapo pia Marekani mkutanoni, ni ufanisi kwa waziri mkuu Al Maliki wa Iraq.

Baada ya ziara kadhaa za kibalozi baina ya nchi hizo mbili-Iran na Iraq, Teheran iliwafiki kumpeleka Sham el Sheikh, waziri wake wa mambo ya nje Mottaki kuhudhuria kikao ambacho ataketi meza moja na waziri wa nje wa Marekani Dr.Condoleeza Rice.

Juzi jumapili, waziri mkuu wa Irak al maliki aliwaonya majirani zake kuwa “ hujuma za kigaidi zinazolenga Iraq hazitaishia Iraq tu, bali zitaenea katika kila nchi duniani.”

Waziri mkuu huyo wa Iraq kutoka madhehebu ya shiia,alizuru Misri,Kuweit na Oman akipiga upatu aungwemkono juhudi zake miongoni mwa viongozi wa madhehebu ya sunni wenye shakashaka na utawala wake mpya unaoonekana unaelemea sana Teheran,mpinzani wao wa jadi katika ghuba.

Iran imepokea mualiko kuhudhuria mazungumzo haya wakati wa mazungumzo ya simu jumapili baina ya waziri mkuu al maliki na rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran.

Iran, ingali imekasirika kwa kuendelea kuwekwa kizuizini kwa maafisa wake 5 wa kibalozi na wanajeshi wa Marekani nchini Iraq kwa tuhuma za kupalilia huko ugaidi.

Saudi Arabia imekwishasema kuwa, waziri mkuu Al Maliki, hatendi ya kutosha kuwajumuisha wajumbe wa madhehebu ya sunni nchini mwake katika utaratibu wa kisiasa.Jumapili, waziri was nje wa Baghdad Zebari alihakikisha ripoti kwamba, mfalme wa saudia alikataa ombi la kuonana na al maliki.

Mvutano baina ya Washington na Teheran, ukiendelea juu ya mradi wa kinuklia wa Iran ,uwezekano wa kukutana kwa waziri wa nje wa Marekani Dr.Condoleeza Rice na waziri wa nje wa Iran,Mottaki, huenda ukagubika macho ya watu hali ya usalama nchini Iraq.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com