Miaka mitano ya vita vya Irak yaadhimishwa leo | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Miaka mitano ya vita vya Irak yaadhimishwa leo

Marekani bado haijatimiza ahadi zake

Sanamu ya Saddam Hussein ikiangushwa katika uwanja wa Firdos mjini Baghdad

Sanamu ya Saddam Hussein ikiangushwa katika uwanja wa Firdos mjini Baghdad

Vita nchini Irak kimsingi havijamalizika rasmi. Lakini inachukuliwa vita hivyo vilimalizika siku kama hii ya leo miaka mitano iliyopita wakati sanamu ya kiongozi wa zamani wa Irak, marehemu Saddam Hussein, ilipoangushwa mjini Baghdad. Jinsi Marekani ilivyoahidi wakati huo na ukweli halisi wa mambo yalivyo nchini Irak ni tofauti.

Tarehe 9 mwezi Aprili mwaka wa 2003 katika mji mkuu wa Irak, Baghdad.

Ni sauti ya watu na kuanguka kwa sanamu ya rais wa zamani wa Irak, hayati Saddam Hussein. Mbele ya kamera za televisheni Wairaki pamoja na Wamarekani walishuhudia kuanguka kwa sanamu hiyo.

Takriban majuma matatu tangu vita vya Irak kuanza wanajeshi wa Marekani walifaulu kuingia katikati ya mji mkuu Baghdad na kuuangusha utawala wa kidikteta wa Irak. Serikali ya Saddam hatimaye ilipoteza udhibiti wa mji huo.

Hisia

Nchi jirani za kiarabu zilishangazwa sana na jinsi utawala wa Saddam ulivyoangushwa kwa haraka. Marekani lakini ilishangilia hata serikali ya mjini Washington ikaonya kwamba wanajeshi wa Irak walikuwa wakikabiliwa na kitisho ambacho kilikuwa bado hakijawatokea.

Makamu wa rais wa Marekani, Dick Cheney, alisema wakati huo.

"Katika mji wa Baghdad asubuhi ya leo tumeona ushahidi wa kuanguka kwa utawala wa ndani wa Saddam Hussein. Barabara zimejaa watu wanaoshangilia. Na ingawa bado kuna maafisa kadhaa wa vikosi vya usalama ambao wamesalia, wanaonekena hawana nguvu ya kuendeleza upinzani."

Dick Cheney und George Bush

Rais George W Bush (kulia) na makamu wake Dick Cheney

Makamu wa rais Dick Cheney alikuwa na maono kwa wakati uliofuata baada ya kuondolewa madarakani Saddam Hussein. Alisema wanajeshi wa Marekani walitakiwa kukaa Irak kama wangelazimika kufanya hivyo.

"Nina matumaini watu wa eneo hilo watatuhukumu kulingana na kitakachotokea Irak kuanzia sasa. Tunataka kwa haraka kuanzisha serikali mpya ya Irak yenye kasi mpya, inayojumulisha Wairak wote na yenye demokrasia. Na tunataka pia kuwaondoa wanajeshi wetu haraka iwezekanvyo. Hatuko nchini Irak kuikalia."

Ukweli kwamba wanajeshi wa Marekani walitakiwa waondoke Irak haraka iwezekanavyo, alithibitisha pia rais wa Marekani, George W Bush. Akiwahutubia moja kwa moja wananchi wa Irak aliwaahidi matatizo yangemalizika.

"Na watu wote wanaoishi nchini mwenu wakiwemo Wakurdi, Washia, Wairaki wenye asili ya kituruki, Wasunni na wengineo, watakuwa huru kutokana na mauaji ya kinyama ambayo wengi wameyavumilia. Janga ambalo Saddam Hussein amelileta nchini mwenu litakwisha hivi karibuni."

Katiba hotuba yake hiyo kwa Wairak, rais Bush aliwasifu sana na kuwaahidi wangekuwa huru.

"Nyinyi ni watu wazuri na wenye vipawa. Warithi wa utamaduni mkubwa unaochangia katika ubinadamu wetu. Mna haki ya kupata vitu vizuri zaidi kuliko udhalimu, ufisadi na vyumba vya mateso. Mna haki kuishi kama watu walio huru na ninamhakikishia kila mwananchi kwamba taifa lenu litakuwa huru hivi karibuni."

Miaka mitano

Leo hii miaka mitano baadaye, Saddam Hussein alikamatwa, akahukumiwa kunyongwa na kweli akatiwa kitanzi mwishoni mwa mwaka wa 2006. Lakini mpaka sasa bado giza limetanda nchini Irak huku Marekani na washirika wake waliosalia katika jeshi la muungano wakijadiliana mara kwa mara kuhusu kuongeza wanajeshi zaidi nchini Irak.

Saddam am Strick

Saddam akitiwa kitanzi

Wanajeshi takriban 300,000 wako Irak, wakiwemo wanajeshi 250,000 wa Marekani. Wanajeshi zaidi ya 4,300 wameuwawa huku idadi ya raia waliouwawa ikikadiriwa kufikia maelfu.

Na tangazo la rais Bush kwamba hakungekuwa tena na vyumba vya mateso imekuwa upuuzi mtupu hususan baada ya kashfa ya wanajeshi wa Marekani kuwatesa wafungwa wa Irak katika jela ya Abu Ghraib.

 • Tarehe 08.04.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DeOI
 • Tarehe 08.04.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DeOI
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com