Mfalme wa Qatar azuru Ujerumani
15 Septemba 2017Katika kituo chake cha kwanza mjini Ankara Alhamisi usiku, Amir huyo wa Qatar alikutana na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye amekuwa muunganji mkono mkubwa wa Qatar wakati wa mzozo wa kidiplomasia uliodumu kwa miezi mitatu sasa, ambao umeiacha Qatar ikiwa imetengwa na jirani zake.
Saudi Arabia, Misri, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu zilivunja uhusiano na Qatar mwezi Juni kuhusiana na ukaribu wake na Iran na madai kwamba taifa hilo dogo tajiri linaunga mkono makundi ya itikadi kali. Qatar inakanusha kuunga mkono itikadi kali, ikisema mgogoro huo ulichochewa kisiasa.
Merkel, Al-Thani waeleza dhamira ya kumaliza mzozo
Wakizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi habri mjini Berlin, Kansela Merkel na Mfalme wa Qatar wameelezea dhamira yao ya kuumaliza mgogoro kati ya Qatar na jirani zake kwa njia za kidiplomasia.
Kansela Merkel amesema haoni suluhu ya haraka kwa mgogoro huo lakini Ujerumani ingependa kusaidia katika utatuzi na kwamba wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na mfalme wa Kuwait kuutatua mzozo huo.
Kwa upande wake, Mfalme Al-Thani amesema yuko tayari kuutatua mzozo huo, na kuongeza kwamba ipo haja ya kuliangalia kwa undani suala la ugaidi. Ameishukuru Ujerumani kwa juhudi zake za usuluhishi. Wawili hao pia wamezungumzia uhusiano wa kimkakati wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Qatar.
Ujerumani imekuwa ikiunga mkono juhudi za kidiplomasia za kuutatuta mzozo huo, na waziri wa mambo ya nchi za nje Sigmar Gabriel amesema idara ya uchunguzi ya Ujerumani itashiriki katika uchunguzi wa madai kwamba Qatar inayasaidia makundi ya kigaidi.
Tofauti za kisera kama kiini cha mgogoro
Mjini Ankara, viongozi hao wawili walisitiza haja ya kutafuta suluhu kupitia njia za kidiplomasia kulingana na ofisi ya Rais Erdogan. Lakini profesa wa masomo ya kanda ya Mashariki ya Kati katika chuo kikuu cha Qatar Mhajoob Zweiri ameelezea tofauti za kisera katika diplomasia za mataifa hayo kuwa kikwazo kikubwa katika kusuluhisha mgogoro huo.
"Saudi Arabia na UAE hiziridhishwi na sera ya kidiplomasia ya Qatar na zilijaribu kulaazimisha sera zao za kidiplomasia zinazowiana na maslahi yao kwa Qatar. huu ndiyo mzizi wa tatizo hilo," alisema msomi huyo.
Maslahi ya Ujerumani Qatar
Qatar, nchi ndogo yenye ukubwa sawa na jimbo la Hessen la hapa Ujerumani na jumla ya wakaazi milioni 2.6, ndiyo inaongoza duniani kwa uzalishaji wa gesi asilia, na inachangia asilimia 30 ya gesi yote inayouzwa kwenye soko la dunia.
Ina umuhimu mkubwa kwa Ujerumani kutokana na ukweli kwamba makampuni karibu 200 ya Ujerumani yana uwakilishi nchini humo na Ujerumani iliuza bidhaa za thamani ya euro bilioni 2.5 nchini Qatar katika mwaka wa 2016.
Qatar pia ni mwekezaji mkubwa katika mashirika kadhaa ya Ujerumani, ikiwemo benki kubwa zaidi ya ukopeshaji - Deutsche Bank, ambamo inamiliki asilimia 6.1 ya hisa kupitia wakfu wake wa uwekezaji wa nje QIA. Pia inamiliki asilimia 15 ya hisa katika kampuni kubwa zaidi ya magari barani Ulaya Volkswagen.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpad,ape.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman