1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merz awasifu viongozi wa EU na kuwarai kuwa wamoja zaidi

29 Januari 2026

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amewatolea wito viongozi wenzake ndani ya Umoja wa Ulaya kuungana, kujizatiti, na kuwa jumuiya yenye nguvu na huru hasa katika wakati huu wa mvutano.

https://p.dw.com/p/57hag
Berlin I Ujerumani
Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: Liesa Johannssen/REUTERS

Akilihutubia bunge la Ujerumani kuhusu sera za kigeni wiki moja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kulegeza ari yake ya kukinyakua kisiwa cha Greenland kilicho chini ya Denmark, Kansela Merz amesema Ulaya ndio "njia mbadala wa ubeberu na utawala wa kimabavu duniani.

Kiongozi huyo amesema Ulaya inahitaji kutafuta njia ya kuwa kiungo muhimu tena ili kujiimarisha licha ya mabadiliko ya nguvu ya kiutawala duniani ambayo yanashuhudiwa  tangu Trump aingie madarakani kwa muhula wa pili zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

"Wiki iliyopita, tulionyesha kwamba sisi katika umoja wa ulaya tunaweza kuchukua hatua haraka sana tunapokuwa na jambo lenye kutia shaka. Tulikubaliana kwamba hatutakubali kutishwa na vitisho vya ushuru wa forodha tena." alisema Merz.

 Berlin 2026 | Friedrich Merz
Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: Liesa Johannssen/REUTERS

Katika hotuba hiyo kwa wabunge,Merz amesema ili Ulaya ijiimarishe, bara hilo lazima lijiamulie usalama wake, kupanua uwezo wake wa ulinzi, kuongeza kasi ya ushindani wake kiuchumi na kuendana na Marekani na China zilizo katika mstari wa mbele.

Merz: Hatutokubali kudharauliwa 

Akizungumzia kauli tata zilizotolewa na rais wa Marekani Donald Trump wiki iliyopita na zilizoonesha umuhimu mdogo wa wanajeshi wa jumuiya ya kujihami ya NATO akirejelea vita vya Afghanistan mwaka 2001, Merz amekosoa matamshi hayo na kusema kwamba hawatokubali kudhauriliwa kwa kuwa walitoa mchango wao kwa mshirika wao huyo.

Katika mahojiano na televisheni ya Marekani yaFox News, Trump alidai kwamba nchi zingine kadhaa za NATO zilituma wanajeshi nchini Afghanistan, lakini "zilikuwa nyuma nyuma wakati wa mapambano.

Merz amesema wanajeshi 59 wa Ujerumani waliuawa katika vita nchini Afghanistan, na kwamba zaidi ya wengine 100 walijeruhiwa vibaya wakati wa misheni hiyo.

 Berlin 2026 |Friedrich Merz
Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: Bernd von jutrczenka/dpa/picture alliance

Lakini katika namna nyingine ametoa wito wa kuimarishwa zaidi kwa jumuiya ya kujihami ya NATO 

 " Muungano wa Ulaya na Marekani na uaminifu wa muungano huo bado ni wa thamani kubwa leo na kwetu sisi Ujerumani una thamani ya kipekee'' amesema Merz.

Katikati ya mpangilio huu wa dunia unaobadilika, Ujerumani inalenga kuwa "sehemu ya mtandao wenye nguvu na  huru ambao unataka kuendelea kufuata utaratibu unaotegemea sheria.