Merkel ziarani Ugiriki | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Merkel ziarani Ugiriki

Kansela wa Ujerumani leo (11.04.2014), anaelekea nchini Ugiriki kama ishara ya kuunga mkono hatua za kubana matumizi zilizochukuliwa na serikali ya nchi hiyo, siku moja baada ya Ugiriki kurejea katika soko la kimataifa.

Samaras akiwa na Kansela Merkel

Waziri Mkuu Samaras akiwa na Kansela Merkel

Ziara hiyo inafanyika huku wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wakionya kuwa Ugiriki bado haijakabiliana sawasawa na mzozo wake wa kiuchumi. Katika ziara hiyo ya siku moja, Kansela Merkel atakutana na Waziri Mkuu wa Ugiriki, Antonis Samaras ambapo watazungumzia hali ya kifedha ya taifa hilo, ahadi za uwekezaji wa miradi pamoja na mipango kazi ya kuwasaidia vijana. Merkel pia anatarajiwa kuhudhuria kongamano la wajasiriamali vijana.

Katika siku za nyuma, Wagiriki wengi walimlaumu Kansela Merkel kwa kusisitiza umuhimu wa Ugiriki kufanya mageuzi ya kiuchumi na kubana matumizi ili kuunusuru uchumi wa nchi hiyo, ambayo imekuwa na rekodi ya ukosefu wa ajira kwa karibu asilimia 28.

Mwaka 2012 Merkel alipofanya ziara mjini Athens, alikabiliwa na maandamano makubwa, lakini katika ziara ya leo, maandamano na mikusanyiko ya hadhara imepigwa marufuku katikati mwa mji wa Athens.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki, Evangelos Venizelos

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki, Evangelos Venizelos

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki, Evangelos Venizelos, anaichukulia ziara hiyo ya Merkel kama ushahidi kwamba nchi yake ''imefungua ukurasa mpya'', katika juhudi za kufanya mageuzi ya kiuchumi.

Akizungumza kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, utakaofanyika kesho Jumamosi (12.04.2014) mjini Athens, Waziri Venizelos, amesema kutokana na Ugiriki kurejea katika masoko ya hisa, Kansela Merkel anataka kuonyesha ishara ya kuunga mkono juhudi za nchi hiyo.

Ugiriki yarejea katika masoko ya hisa

Jana Alhamisi (10.04.2014), Ugiriki ilifanikiwa kuongeza Euro bilioni tatu katika masoko ya hisa ya kimataifa. Mauzo hayo ya dhamana ni ya kwanza tangu Ugiriki ilivyofungiwa katika masoko ya kimataifa mwaka 2010, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu hali yake ya kifedha.

Katika kipindi hicho takwimu zilionyesha kuwa deni la taifa la Ugiriki lilikuwa kubwa kuliko ilivyokisiwa awali. Kutokana na hali hiyo, Ugiriki imekuwa ikitegemea msaada wa kimataifa kuunusuru uchumi wake.

Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya kiuchumi, George Tzogopoulos, wa mfuko wa Ulaya na Sera za Kigeni-ELIAMP, anaonyesha shauku kwa kusema ni muhimu Ugiriki kuzingatia makubaliano iliyofikia ili kuweza kurejesha tena imani yake katika masoko ya hisa.

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani

Tzogopoulos anasema masoko hayo yanaweza kuona kuwa hatua ya Ujerumani kuiunga mkono Ugiriki, ni kama hakikisho la mkopo kwa nchi hiyo, hasa tangu ilivyoahidi kufanya mageuzi ya kiuchumi ambayo tayari imeanza kuyatekeleza, ingawa anasema bado mfano wa kisiasa haujitoshelezi.

Viongozi wa ngazi ya juu kabisa wa Ujerumani wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mchakato wa mageuzi ya kiuchumi ya Ugiriki. Mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Rais Joachim Gauck alizuru Ugiriki. Ziara kama hiyo ilifanywa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DW,DPAE
Mhariri: Gakuba Daniel

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com